1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi yakosolewa kuandaa uchaguzi katika maeneo ya Ukraine

18 Machi 2024

Umoja wa Ulaya umeikosoa Urusi kufanya uchaguzi katika maeneo iliyoyanyakuwa kutoka UKraine baada ya Moscow kutangaza kuwa rais wa Urusi ameshinda uchaguzi huo kwa kishindo.

Ukraine, Luhansk  | Uchaguzi wa Urusi 2024
Tume ya Uchaguzi Urusi imesema watu takriban milioni 76 wamempigia kura Putin na kuumpa ushindi wa asilimia 88 ya kura. Picha: Alexander Reka/TASS/dpa/picture alliance

Taarifa ya Mkuu wa sera za  nje ya  Umoja huo wa Ulaya Josep Borrell, imesema wanakosoa hatua isiyo halali ya kufanyika uchaguzi huo katika maeneo ya Ukraine yaliyonyakuliwa na Urusi katika jimbo la Crimea, lililonyakuliwa mwaka 2014 kinyume cha sheria ya kimataifa. Maeneo mengine yaliyoshiriki uchaguzi ni pamoja na  jimbo la Donetsk, Luhansk, Zaporizhzhya na Kherson.

Umoja huo umesema hautatambua uchaguzi uliofanyika katika maeneo hayo wala matokeo yake. Umeongeza kuwa uchaguzi haukuwa huru wala wa haki na hauwezi kuleta mabadiliko yoyote ya halali.

"Nataka kusema kwamba huu haukuwa uchaguzi wa huru na haki, hapakuwa na waangalizi wa shirika la usalama na ushirikiano barani  Ulaya OSCE, mazingira hayakuwa mazuri, hiki ndicho nnachoweza kusema, lakini zaidi ya hilo uchaguzi ulikuwa wa ukandamizaji na vitisho na kufanyika katika maeneo yalionyakuliwa na hatua hii inakiuka uhuru wa Ukraine," alisema Borrell.

Ushindi wa Rais Putin wazua hisia mseto duniani

Kiongozi wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny anaedaiwa kuuwawa na utawala wa nchi hiyo siku chache kabla ya Uchaguzi Mkuu Picha: Dmitri Lovetsky/AP/picture alliance

Taarifa hiyo ya Umoja wa Ulaya pia imesema mauaji ya kushtusha ya kiongozi Mkuu wa upinzani wa Urusi aliyekuwa mpinzani mkubwa wa Rais Putin, Alexei Nalavy siku chache kabla ya uchaguzi, ni ishara ya kuongezeka kwa mfumo wa ukandamizaji. 

Ujerumani kupitia Waziri wake wa mambo ya kigeni Annalena Baerbock, imesema uchaguzi huo ambao haukutoa nafasi, watu kumchagua rais wamtakae inaonesha tabia ya uonevu aliyonao Putin kwa raia wake. Ufaransa nayo imesema masharti ya kufanyika uchaguzi huru Urusi hayakutimizwa.

Urusi inafanya uchaguzi katikati ya vita na Ukraine

Imesema uchaguzi umefanyika wakati kukiwa na ukandamizaji unaoongezeka dhidi ya mashirika ya kiraia na upinzani unaodhibitiwa na utawala uliopo huku ikiwasifia warusi waliopinga kile walichokiita shambulio la haki yao ya kisiasa.

David Cameron, waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereua amesema uchaguzi uliofanyika umeonesha namna utawala wa Putin unavyopania kuunyamazisha upinzani dhidi ya vita vyake visivyohalali nchini Ukraine. Moldova na Norway pia zilijiunga katika msururu wa kuukosoa uchaguzi wa Urusi.

India yasema yatarajia kuimarisha zaidi mahusiano yake na Urusi

Rais wa Urusi Vladimir Putin akiwa na Waziri Mkuu wa India Narendra ModiPicha: Alexandr Demyanchuk/SPUTNIK/AFP

Wakati Putin akiendelea kukosolewa na mataifa ya Magharibi, kwengineko duniani ameendelea kupongezwa kwa ushindi mnono alioupata baada ya kumalizika uchaguzi uliodumu siku tatu kuanzia tarehe 15 hadi 17 Machi. Waziri Mkuu wa India  Narendra Modi amesema anategemea kuimarisha zaidi mahusiano ya mataifa hayo mawili kwa miaka ijayo.

Urusi inaendelea kuwa mshirika muhimu inayoiuzia silaha India taifa lililo na idadi kubwa ya watu. India hadi sasa imekataa kuikosoa Urusi dhidi ya uvamizi wake Ukraine hata wakati inapojaribu kutafuta ushirikiano zaidi wa kiusalama na Marekani.

Putin aweka rekodi kwenye matokeo ya uchaguzi Urusi

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un hakuachwa nyuma katika salamu za kumpongeza Putin kwa ushindi wa kishindo, akisema nchi yake itafanya kazi nae kuendeleza mahusiano ya mataifa hayo mawili. Kulingana na shirika la habari la taifa KCNA Kim Jong Un ataungana pamoja wakati huu kutoa nafasi nyengine ya kuimarika kwa urafiki wao wa kihistoria ili kujenga mataifa yaliyoimara.

Awali Mkuu wa Tume ya Uchaguzi Urusi Ella Pamfilova alisema takriban watu milioni 76 wamempigia kura Putin na kuumpa ushindi wa asilimia 88 ya kura.

Putin ashinda uchaguzi wa rais

01:34

This browser does not support the video element.

dpa/ap/reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW