1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine: Shirika la OSCE lailaumu Urusi kwa kukiuka sheria.

Zainab Aziz Mhariri: Daniel Gakuba
13 Aprili 2022

Ripoti ya shirika kubwa zaidi la usalama duniani OSCE inailaumu Urusi kwa vitendo vya ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu nchini Ukraine.

Österreich | OSZE-Sitzung im Zeichen der Krisendiplomatie mit Russland
Picha: Michael Gruber/Getty Images

Ripoti hiyo iliyochapishwa na Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya (OSCE) imesema iwapo Urusi ingeheshimu majukumu yake ya kimataifa baada ya kuivamia Ukraine mnamo Februari 24, idadi ya raia waliouawa au waliojeruhiwa ingekuwa ya chini zaidi. Ripoti ya kurasa 110 iliwasilishwa kwenye mkutano wa baraza la kudumu la OSCE.

Maandalizi kabla ya kutangazwa ripoti ya shirika la OSCE.Picha: Alexey Vitvitsky/Sputnik/dpa/picture alliance

Shirika hilo lina wanachama 57 katika mabara matatu ikiwa ni pamoja na Urusi, Ukraine na Marekani. Katiba ya shirika hilo inaruhusu kuundwa jopo la dharura la wataalam ili kusaidia katika kutatua matatizo ya nchi wanachama lakini Urusi ilikataa kuchangia katika ripoti hiyo na kulingana na wataalamu wake, utaratibu huo umepitwa na wakati na haufai kutumika.

Wakati huo huo Rais wa Marekani Joe Biden amesema uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ni sawa na "mauaji ya halaiki," huku akimtuhumu Rais Vladimir Putin kwa kujaribu kufuta wazo la mtu kuwa raia wa Ukraine. Msemaji wa ikulu ya Urusi, Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa habari kwamba tamko hilo la Biden halikubaliki na kwamba Urusi haikubaliani na jaribio lolote la kupotosha hali halisi.

Rais wa Marekani Joe Biden.Picha: Carolyn Kaster/AP/picture alliance

Mengine kuhusu vita vya nchini Ukraine: Rais Volodymyr Zelensky analitaka bara la Ulaya lichukue hatua zaidi dhidi ya Urusi, akionya kwamba bila nchi hiyo kuzuiwa italichukua eneo lote la Ulaya Mashariki.

Ujerumani kwa upande wake kwa sasa imekataa kutii marufuku ya Umoja wa Ulaya juu ya ununuzi wa mafuta na gesi ya Urusi lakini pia inaendelea kupinga malipo kwa bidhaa hizo kwa kutumia sarafu ya Urusi ya Ruble. Msemaji wa wizara ya uchumi amesema kampuni za Ujerumani zinaendelea kutumia sarafu ya Euro kulipia gesi kutoka Urusi.

Mkurugenzi mkuu wa chama cha viwanda vya karatasi Alexander von Reibnitz amesema marufuku ya gesi kutoka Urusi maana yake ni kusimamishwa kwa uzalizashi wa karatasi nchini Ujerumani kote. Amesema kupiga marufuku kuagiza gesi kutoka Urusi kwa sababu ya uvamizi wake nchini Ukraine kutasababisha madhara katika sekta ya uzalishaji wa karatasi nchini Ujerumani.Von Reibnitz amesema vita vya nchini Ukraine tayari vimeshawaathiri watengenezaji wa karatasi kutokana na bei kubwa za  malighafi.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz.Picha: BEN STANSALL/Pool/AFP

Naye mwenyekiti wa bodi ya viwanda vya usindikaji malighafi Steffen Würth ameeleza kuwa athari za vita sasa zinazidi kuilemea sekta ya viwanda vya karatasi nchini Ujerumani. Marufuku ya gesi kutoka Urusi itaathiri uzalisahji wa chakula, ufungaji wa dawa, mali ghafi za kutengeneza dawa na pia utengenezaji wa karatasi maalumu kama vile mirija. Karatasi kwa ajili ya sekta ya  vyombo vya habari na uenezi pia itaathirika ikiwa gesi kutoka Urusi itapigwa marufuku.

Na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR limesema zaidi ya wakimbizi 40,000 wa Ukraine wameikimbia nchi hiyo katika muda wa saa 24. UNHCR imetahadharisha juu ya wafanyabiashara haramu wanaotaka kuwadhukumu hasa wanawake na watoto walio katika mazingira magumu katika hatua za kukimbia vita.

Wakimbizi kutoka Ukraine.Picha: Armend Nimani/AFP/Getty Images

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema raia wa Ukraine wapatao 4,656,509 wameikimbia nchi yao tangu Urusi ilipoivamia Februari 24 na kwamba wanawake na watoto ni asilimia 90 ya wale ambao wameondoka Ukraine. Kamishna mkuu msaidizi wa UNHCR Gillian Triggs amesema mgogoro wa wakimbizi wa Ukraine ni mgogoro unaohusiana na ulinzi kwa wanawake na watoto.

Vyanzo: DPA/AP/RTRE/AFP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW