Urusi yalaumu Magharibi kwa mzozo kati yake na Ukraine
8 Mei 2024Urusi imesema kuwa mzozo kati yake na Ukraine ungeisha katika muda wa wiki mbili iwapo mataifa ya Magharibi yangesitisha kuipatia silaha Ukraine, ikirejelea kauli iliyotolewa na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borell.
Soma pia: Urusi yakemea pendekezo la kutumia mapato ya mali zake zilizozuiwa
Mapema mwezi huu, Borell alieleza kuwa uwepo wa Ukraine unategemea mataifa ya Magharibi na kwamba vita vyake na Urusi vingemalizika katika wiki chache tu iwapo mataifa ya Magharibi yangelizuwia kuipa Ukraine silaha. Hata hivyo, Borell hakutaka vita hivyo vikamilike kwa namna hiyo.
Alipoulizwa kuhusu jinsi ya kupunguza mzozo kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Urusi, Maria Zakharova, amesema mataifa ya Magharibi yanapaswa kuizingatia kauli ya Borell.