1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yalenga kituo cha treni Ukraine na kuwaua watu 25

Sylvia Mwehozi
25 Agosti 2022

Raia 25 wa Ukraine wameuawa kwenye shambulio la kombora la Urusi ambalo lilisababisha treni ya abiria kuwaka moto mashariki mwa nchi hiyo.

Ukraine-Krieg Tschaplyne | russischer Angriff auf Bahnhof
Picha: Dmytro Smolienko/Ukrinform/IMAGO

Shambulio hilo lilitokea hapo jana wakati nchi hiyo ilipokuwa inaadhimisha siku ya uhuru. Katika ujumbe wake kwa njia ya video alioutoa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema kuwa mashambulizi ya maroketi yameipiga treni ya abiria katika mji mdogo wa Chaplyne, ulioko kilometa 145 magharibi mwa mji unaodhibitiwa na Urusi wa Donetsk.

"Chaplino ni maumivu yetu leo. Kufikia wakati huu, kuna watu 22 waliokufa, ikiwa ni pamoja na watu watano ambao waliochomwa kwenye gari. Kijana aliyekuwa na umri wa miaka 11 amekufa, roketi la Urusi liliharibu nyumba yake."

Zelensky alikuwa tayari ameonya juu ya kitisho cha "uchochezi wa kuchukiza wa Urusi" kuelekea maadhimisho ya miaka 31 ya Uhuru yaliyofanyika siku ya Jumatano kutoka utawala wa kisovieti ulioongozwa na Moscow ambapo sherehe za umma zilifutwa.

Maadhimisho hayo yaligongana na kumbukumbu ya miezi sita tangu vikosi vya Urusi vilipoivamia Ukraine na kuibua mzozo mkubwa barani Ulaya tangu vita vya pili vya dunia. Mshauri wa rais wa Ukraine Oleksiy Arestovych alisema kuwa vikosi vya Urusi viliepuka kushambulia mji mkuu wa kyiv wakati wa maadhimisho hayo na badala yake vikaelekeza mashambulizi ya mizinga katika miji ya Kharkiv, Mykolaiv, Nikopol na Dnipro.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken aliandika pia kupitia ukurasa wa Twitter kwamba "shambulio la kombora la Urusi dhidi ya kituo cha treni kilichokuwa na umati wa raia nchini Ukraine linafaa kuwa mfano wa ukatili". Blinken amesisitiza kwamba Marekani na washirika wake wataendelea kusimama na Ukraine na kusaka uwajibikaji dhidi ya maafisa wa Urusi.Watu 25 wauawa katika shambulizi la kituo cha treni Ukraine

Rais Zelensky na Waziri mkuu Boris Johnson Picha: Andrew Kravchenko/AP Photo/picture alliance

Kulikuwa na milipuko mingine sita wakati wa shambulio hilo la roketi katika mkoa wa Vyshgorod ulioko kaskazini mwa mji mkuu wa Kyiv, lakini mamlaka za mji huo zimesema kwamba hapakuwa na maafa yoyote kwa maana ya uharibifu wa majengo na miundombinu.

Naye mkuu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amemtaka rais wa Urusi Vladimir Putin kusimamisha mashambulizi ya silaha dhidi ya Ukraine na kusema kwamba vikosi vya kijeshi vinapaswa kuondolewa katika eneo la kinu cha nyukilia cha Zaporizhzhia. Ameongeza kuwa "jumuiya ya kimataifa lazima isisitize juu ya kurekodiwa kwa matukio hayo" ili siku moja yaweze kuthibitisha uhalifu wa kivita. Bachelet ametoa kauli hiyo katika hotuba ya kuhitimisha muhula wake kama kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW