Urusi yamfunga jela mwandishi habari wa Marekani Kurmasheva
23 Julai 2024Hukumu hiyo ilitolewa kwa Kurmasheva wakati wa kesi ya faragha iliyofanyika katika mji wa Kazan wa kusini magharibi mwa Urusi. Kurmasheva, ambaye ana umri wa miaka 47, aliifanyia kazi Radio Free Europe/Radio Liberty - RFE/RL, inayofadhiliwa na serikali ya Marekani.
Mahakama ya Urusi ilimtuhumu Kurmasheva kwa kusambaza habari za uwongo kuhusiana na ripoti zake za vita vinavyoendelea Ukraine. Rais wa RFE/RL Stephen Capus aliita kesi hiyo ya Urusi kuwa ni dhihaka kwa mkondo wa sheria. Kifungo cha mwandishi habari huyo mwanamke kinajiri siku chache tu baada ya mwandishi habari Mmarekani Evan Gershkovich kuhukumiwa kifungo cha miaka 16 jelanchini Urusi. Gershkovich, aliyelifanyia kazi jarida la Wall Street, alihukumiwa kwa mashitaka ya ujasusi. Marekani ilisema mashitaka hayo dhidi ya Gershkovich yalichochewa kisiasa na serikali ya Urusi.