1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaongeza mashambulizi Donbas, mashariki mwa Ukraine

24 Mei 2022

Vikosi vya Urusi leo Jumanne vimeongeza mashambulizi yao kwenye eneo la mwisho la upinzani karibu na jimbo la Lugansk, katika eneo la Donbas mashariki mwa Ukraine wakati vita hivyo vikiingia mwezi wake wa nne.

Bilderchronik des Krieges in der Ukraine
Jengo la chuo kikuu lililoharibiwa na shambulio la roketi mjini BakhmutPicha: Carlos Barria/REUTERS

Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwishoni mwa mwezi Februari, uungwaji mkono wa nchi za Magharibi kwa kiasi kikubwa imeisadia Ukraine kudhibiti vikosi vya Urusi- ikiwemo kuwazuia wanajeshi wake kuchukua udhibiti wa mji mkuu wa Kyiv- lakini kwa sasa Urusi inalenga kulitia mikononi mwake eneo zima la Donbas na eneo la pwani ya kusini. 

Jeshi la Ukraine kupitia ukurusa wake wa Facebook limesema leo kuwa vikosi vya Urusi vinafanya mashambulizi makali katika eneo la Donbas.

Soma pia: Scholz atetea uamuzi wa kuipatia Ukraine silaha

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi Igor Konashenkov amesema, "Makombora ya masafa marefu ya anga yalishambulia na kuharibu mabohari matatu ya silaha za kijeshi, sehemu ya kuhifadhi bunduki na maghala kadhaa ya risasi katika maeneo ya Minkivka, Bakhmut, na Spirne."

Gavana wa jimbo la Lugansk ameongeza kuwa Urusi imetuma maelfu ya wanajeshi wake katika jimbo hilo ili kuliteka na kwamba mji wa Severodonetsk pia ulikuwa chini ya mashambulizi. Gavana huyo amewataka waakazi katika maeneo hayo kuhama.

Vikosi vya Urusi vinaripotiwa kulekeza nguvu zao zote katika maeneo ya mashariki mwa Ukraine hasa baada ya kuutia mikononi mji wa bandari wa Mariupol siku chache zilizopita.

Urusi imerusha makombora 1,500 na kufanya mashambulizi 3,000 ya anga

Wanajeshi wa Ukraine wakishika doria karibu na eneo la DonetskPicha: Alex Chan Tsz Yuk/SOPA Images/ZUMA Press/picture alliance

Ukraine ina wasiwasi juu ya ongezeko la mashambulizi katika maeneo hayo ya mashariki hasa kutokana na uwepo wa viwanda na migodi ya makaa.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika hotuba yake ya jana usiku baada ya viongozi wa serikali za mitaa na wakaazi kuripoti kushadidi kwa mashambulizi ya mabomu, alisema "Wiki zijazo za vita zitakuwa ngumu, lazima hilo tulifahamu. Hali ni mbaya sana katika eneo zima la Donbas, na maeneo yaliyoathirika Zaidi ni miji ya Bakhmut, Popasna na Severodonetsk.”

Soma pia: Urusi: Mamia ya askari wa Ukraine wamejisalimisha

Katika hotuba yake, Zelensky amesema Urusi imerusha takriban makombora 1,500 na kufanya zaidi ya mashambulizi 3,000 ya anga katika miezi mitatu ya kwanza ya vita hivyo.

Rais huyo amewatahadharisha wasomi waliokusanyika katika kongamano la kiuchumi la dunia linalofanyika Davos, Uswizi- ambalo Urusi imezuiwa kushiriki- kwamba ucheleweshwaji wa misaada ya kijeshi una madhara makubwa kwa raia wa Ukraine wanaoendelea kupoteza Maisha.

Amnesty: Urusi imefanya uhalifu Ukraine

01:01

This browser does not support the video element.

Amesema watu 87 wameuawa katika shambulio la Urusi mapema mwezi huu kwenye kambi ya jeshi kaskazini mwa nchi hiyo, shambulio hilo likitajwa kuwa miongoni mwa mashambulizi mabaya zaidi yaliyorekodiwa tangu kuanza kwa vita hivyo.

Nchi za magharibi zimetuma msaada wa kijeshi na fedha kwa Ukraine ili kuisaidia katika mapambano yake na Urusi, huku Moscow ikiwekewa vikwazo chungunzima vya kiuchumi.