1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaongeza mashambulizi Mashariki mwa Ukraine

23 Mei 2022

Hukumu katika kesi ya kwanza ya uhalifu wa kivita kwenye mgogoro kati ya Urusi na Ukraine, ikitarajiwa Jumatatu, mashambulizi ya Urusi Mashariki mwa Ukraine yanazidi kuwa makali

Ukraine  Bakhmut Zerstörter Uni Campus
Picha: Carlos Barria/REUTERS

Kesi mjini Kyiv  inayoonekana kama jaribio la hadharani la uhuru wa mfumo wa mahakama wa Ukraine  inakuja wakati taasisi za kimataifa zikifanya uchunguzi wao wenyewe kuhusu madai ya dhuluma ambazo zimegeuza miji kama Bucha na Mariupol nchini humo kuwa vielelezo vya uharibifu.

Rais wa Poland Andrzej Duda, ambaye nchi yake ni eneo muhimu la usafirishaji wa silaha za mataifa ya Magharibi na hifadhi ya mamilioni ya wakimbizi wa vita, hapo jana alitaja  uharibifu katika miji hiyo kama sababu kwa nini ushirikiano wa kawaida na Urusi hauwezekani tena. Duda ameliambia bunge la Ukraine kwamba ulimwengu wenye uaminifu hauwezi kurejea katika uhusiano wa kawaida huku ukisahau uhalifu, uchokozi na haki za kimsingi zilizokiukwa.

Urusi yaendeleza mashambulizi Donbas

Miezi mitatu baada ya kuanzisha uvamizi ambao umeshindwa katika lengo lake la awali la kuuteka mji wa Kyiv, vikosi vya Urusi sasa vimejikita katika kuongeza na kupanua ufanisi wao katika eneo la Donbas na katika pwani ya kusini mwa Ukraine. Lakini mashambulio makali yakiendelea, mjumbe  mkuu wa Urusi katika mazungumzo , alisema jana kwamba taifa hilo liko tayari kuanzisha tena mazungumzo na Ukraine, ambayo Urusi inailaumu kwa kukwamisha mazungumzo ya awali. Kwa mujibu wa msimamizi wa shughuli za ofisi ya rais wa rais Volodymyr Zelensky, Andriy Yermak,  aliyeandika ujumbe katika mtandao wa twitter kwamba vita hivyo vinapaswa kumalizika kwa kudumishwa kikamilifu kwa uadilifu wa kimipaka wa Ukraine, amesema mazungumzo yoyote hata hivyo hayatajumuisha makubaliano kuhusu ardhi.

Mkuu wa shirika la UNHCR - Filippo GrandiPicha: Lev Radin/Pacific Press/picture alliance

Wakati huo huo, Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR limesema kuwa idadi ya watu waliolazimika kukimbia migogoro, ghasia, ukiukwaji wa haki za binadamu na mateso sasa imevuka watu milioni 100 kwa mara ya kwanza hali iliyochochewa na vita vya Ukraine na migogoro mingine mibaya. Katika taarifa, UNHCR imesema kuwa idadi hiyo ya kushtua inapaswa kuufanya ulimwengu kumaliza mizozo inayolazimisha idadi kubwa ya watu kukimbia makazi yao.

Urusi iliivamia Ukraine Februari 24 na tangu wakati huo zaidi ya watu milioni nane wamekimbia makazi yao ndani ya nchi hiyo, huku zaidi ya wakimbizi milioni sita wakikimbilia mataifa ya nje.

Mkuu wa shirika hilo la UNHCR Fillipo Grandi amesema kuwa idadi hiyo ya watu milioni 100 ni ya kutisha na kushtua na haikupaswa kufikiwa. Grandi ameongeza kuwa hali hii inapaswa kuchochea kutatua na kuzuia migogoro  ya uharibifu, kumalizwa kwa mateso na kushughulikia sababu za msingi zinazowalazimisha watu wasio na hatia kukimbia makazi yao.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW