1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi yaongeza mashambulizi Ukraine na kuuwa watu wanne

Hawa Bihoga
2 Januari 2024

Urusi imefanya mashambulizi makali ya makombora na ndege zisizokuwa na rubani katika mji mkuu Ukraine Kyiv, na kaskazini mashariki mwa mji wa Kharkiv na kuuwa watu wanne na kujeruhi wengine zaidi ya tisini.

Kyiv, Ukraine | Waokoaji wakizima moto baada ya makombora ya Urusi kupiga majengo ya makaazi.
Kikosi cha uokoaji kipambana kuzima moto katika majengo ambayo yamewaka moto baada ya Urusi kushambulia.Picha: Efrem Lukatsky/AP/picture alliance

Mamlaka Ukraine imesema mashambulizi hayo yamesababisha maelfu ya watu kukosa umeme, kutokana na miundombinu kushambuliwa. Moscow imesisitiza kuwa itazidisha mashambulizi dhidi ya Ukraine hadi kufanikisha lengo lake.

Mashambulizi hayo yaliopiga miundombinu ya kiraia yanafanyika chini ya saa 24 tangu rais wa Urusi Vladimir Putin  kusema kwamba, shambulio la anga mjini Belgorod liliuwa watu 24 na kuishutumu Ukraine kutekeleza, huku akiapa kulipiza kisasi kwa kuzidisha mashambulizi hasa katika maeneo ya kimkakati Ukraine.

Meya wa mji wa Kyiv  Vitali Klitschko alisema mwanamke mmoja aliejeruhiwa vibaya baada ya shambulio, alifariki katika gari la wagonjwa wakielekea katika matibabu. Hapo awali alisema kwambatakriban watu kumi na sita walijeruhiwa.

Ameongeza kuwa wakaazi katika wilaya kadhaa katika mji mkuu Kyiv wamekosa huduma muhimu za kijamii ikiwemo maji na nishati ya umeme na gesi, huku kikosi cha uokoaji kikipambana kuzima moto katika maeneo kadhaa baada ya mashambulizi.

Hata hivyo kabla ya mashambulizi tahadhari ya uvamizi wa anga katika mji mkuu kyiv ilidumu karibu kwa saa nne.

Soma pia:Putin ataja shambulizi katika mji wa Belgord kuwa ''tukio la kigaidi''

Nako katika mji wa Mashariki wa Kharkiv Mkuu wa utawala wa kijeshi wa mji huo, Oleg Sinegubov, amesema mwanamke mmoja aliwawa na wengine arobaini na moja walijeruhiwa katika mashambulizi manneambayo yaliharibu majengo ya makaazi. Jeshi la anga la Ukraine limesema Urusu imevurumisha makombora aina ya Kinzhal

Rais wa Urusi Vladimir Putin ameapa kuwa Moscow itazidisha mashambulizi dhidi ya maeneo ya kijeshi nchini Ukraine, baada ya shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa la Ukraine mwishoni mwa juma katika mji wa Belgorod nchini Urusi, ambalo lilisababisha vifo vya watu 25 wakiwemo watoto watano.

"Tutaendelea kushambulia, na leo tutaendelea tukijibu mapigo zaidi na kesho pia." Alisema Putin alipokutana na baadhi ya viongozi wake wa kijeshi.

Zelenskiy: Urusi imezidisha mashambulizi ya anga Ukraine 

Kupitia mtandao wa Telegram rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema kwamba, Urusi imevurumisha takriban ndege zisizo na ruban 170 aina ya "Shahed" zilizotengenezwa nchini Iran na makombora kadhaa tangu Desemba 31.

Ujerumani: Hatutaiacha Ukraine kwenye vita peke yake

02:23

This browser does not support the video element.

Zelenskiyameongeza kwamba kwa siku tatu mfululizo kikosi cha ulinzi wa anga, kimekuwa kikifanya kazi kubwa katika kukabiliana na mashambulizi hayo.

Urusi imeongeza mkururo wa mashambulizi ya anga  nchini Ukraine katika sherehe za mwaka mpya, na siku ya Ijumaa ilifanya shambulio kubwa zaidi la anga kushuhudiwa tangu kuzuka kwa vita hivyo takriban miaka miwili iliopita na kusababisha vifo vya watu takriban 39.

Soma pia:Putin amekuwa vitani kwa zaidi ya miaka miwili sasa na Ukraine huku akiyadhibiti baadhi ya maeneo nchini humo

Kufuatia mashambulizi hayo Poland imesema imetuma ndege nne za kivita chapa F-16 katika mpaka wake na Ukraine leo kwa ajili ya kulinda anga lake.

Poland ambayo ni mwanachama wa NATO na mshirika wa karibu wa Ukraine, imeongeza kuwa mifumo yake ya rada inaonesha kwamba kombora la Urusi la siku ya Ijumaa lilipita katika anga lake kwa umbali wa dakika tatu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW