1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yafanya mashambulizi nchini Ukraine kote

8 Januari 2024

Urusi kwa mara nyingine tena imeishambulia Ukraine kwa makombora. Vyombo vya habari vya Ukraine vimeripoti kutokea milipuko katika maeneo ya mji wa Dnipro ulio kusini-mashariki mwa Ukraine na katika miji mingine.

Russland Belgorod | Schäden nach Beschuss
Picha: Yevgeny Silantyev/Tass/picture alliance

Urusi imeendeleza mashambulizi makali dhidi ya Ukraine ambapo pia mikoa ya mashariki iliyo karibu na mstari wa mbele wa mapigano pamoja na maeneo ya kati na magharibi mwa nchi hiyo yameshambuliwa kwa makombora.

Watu wamekimbilia kwenye kituo cha treni katika jiji la Kiyv nchini Ukraine baada ya kutolewa tahadhari ya uvamizi wa anga, wakati Urusi ikiendeleza mashambulio ya makombora. Januari 8, 2024.Picha: Alina Smutko/REUTERS

Takriban watu watatu wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika wimbi jipya la mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine kote. Naibu mkuu wa ofisi ya rais, Oleksiy Kuleba, amesema watu wawili wameuawa katika mikoa ya Khmelnytskyi na Dnipropetrovsk, na mwingine aliripotiwa kuuawa katika mkoa wa Kharkiv.

Soma Pia:Miji miwili ya Ukraine yashambuliwa na makombora ya Urusi

Meya wa jiji la Kharkiv, Ihor Terekhov, amesema takriban makombora manne yalipiga jiji hilo la pili kwa ukubwa nchini Ukraine. Taarifa zaidi zinafahamisha kuwa mji wa Dnipropetrovsk ndio uliokabiliwa na mashambulizi kwa kiwango kikubwa.

Jengo la makazi pia limeharibiwa katika eneo la kusini mwa Ukraine katika mji wa Zaporizhzhya. Kulingana na mkuu wa jeshi katika mkoa huo Yuri Malashko, kufikia sasa watu wanne wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo makombora ambayo yamesababisha jumla ya milipuko mitano mikubwa katika jiji hilo la Zaporizhzhya.

Jengo lililoharibiwa katika shambulio la roketi la Urusikatika mji wa Zaporizhzhya, Ukraine kwenye mashambulizi ya Jumapili, Januari, Mosi, 2023.Picha: Andriy Andriyenko/AP Photo/picture alliance

Jeshi la Ukraine limesema Urusi imetumia makombora ya masafa marefu aina ya Kinzhal na ndege zisizokuwa na rubani  kushambulia baadhi ya maeneo nchini Ukraine. Tahadhari za uvamizi wa anga zilitolewa kote nchini Ukraine.

Majeshi ya Urusi na ya Ukraine yamekuwa katika vuta nikuvute ambapo kila upande unapambana kuharibu vituo vya kijeshi na miundombinu muhimu ya mwenzake kwa kufanya mashambulizi yanayolenga maeneo mengi, hayo ni kulingana na ripoti ya hivi punde ya vita hivyo vya Ukraine.

Soma Pia:Poland yataka Ukraine ipatiwe makombora ya masafa marefu

Urusi kwa upande wake imewahamisha takriban wakaazi 300 kutoka kwenye mji wa Belgorod, ulio karibu na mpaka wa Ukraine, kutokana na mashambulizi ya Ukraine.  Gavana wa jimbo hilo Vyacheslav Gladkov, amesema watu hao kwa sasa wapo kwenye makazi ya muda katika wilaya za Stary Oskol, Gubkin na Korochansky ambazo ziko mbali na maeneo ya mpakani.

Rais wa Urusi Vladimir Putin, alipozungumza kwenye mkutano wa kila mwaka na waandishi wa habari mjini Moscow, Urusi Desemba 14, 2023Picha: Alexander Zemlianichenko/REUTERS

Katika hali inayoashiria kuongezeka kwa wasiwasi katika eneo la mpakani, viongozi wa eneo hilo wameahirisha shule kufunguliwa kutoka Januari 9, hadi Januari 19.

Vyanzo: DPA/AFP/DW

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW