Urusi yaongeza mashambulizi yaliyoilenga Kyiv
30 Julai 2026
Milipuko imesikika mjini Kyiv mapema leo, kwa mujibu wa mwandishi wa AFP, baada ya Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, kuonya kuwa huenda Urusi ikafanya shambulio jingine kubwa usiku wa kuamkia leo.
Meya wa mji wa Kyiv Vitali Klitschko amesema kuwa Moscow inafanya mashambulizi kwa kutumia makombora ya balistiki huku akiwataka waakazi wa mji ho kutafuta hifadhi katika maakazi salama.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X, Zelensky amesema "Warusi wamejiandaa kufanya shambulio kubwa kwa siku kadhaa, na kuna uwezekano mkubwa kwamba litafanywa usiku wa leo."
Kiongozi huyo pia alirudia wito wake kwa washirika wa Ukraine kuipatia Kyiv silaha zaidi ikiwemo makombora ya kujihami angani ambayo kwa sasa yamepungua pakubwa.
Mnamo siku ya Jumanne, Zelensky alikutana na Rais wa Marekani, Donald Trump, katika Ikulu ya White House, ambako viongozi hao walijadili uwezekano wa Ukraine kutengeneza makombora ya kukinga mashambulizi ya mfumo wa Patriot.