1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi yaonyesha kuwa hali ya kawaida imerejea baada ya uasi

26 Juni 2023

Urusi inajaribu kuonyesha kwamba hali imerejea kuwa ya kawaida Jumatatu baada ya uasi uliojitokeza mwishoni mwa wiki

Russland l Videostill, russische Verteidigungsminister Sergej Schoigu
Picha: Russian Defence Ministry/dpa/picture-alliance

Kitisho hicho cha uasi uliodumu kwa saa kadhaa siku ya Jumamosi kuliongozwa na kiongozi wa mamluki wa Wagner Yevgeny Prigozhin. Tukio hilo linadaiwa kuyumbisha udhibiti wa madaraka wa rais wa Urusi Vladimir Putin.

Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu, alionekana kwenye kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali, akiwatembelea wanajeshi wake nchini Ukraine. Shoigu ni miongoni mwa wale ambao kiongozi wa mamluki wa Wagner Yevgeny Prigozhin, aliwalenga kwenye uasi wake.

Soma pia: Putin anaimani na mipango ya operesheni dhidi ya Ukraine

Wakati wa mkutano wake na wanajeshi, wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema Shoigu alitilia mkazo kile alichokiita "ufanisi mkubwa katika kugundua na kuharibu" mifumo ya silaha ya wanajeshi wa Ukraine.

Maafisa mjini Moscow na katika jimbo la Voronezh kusini mwa mji mkuu, waliondoa mikakati ya hali ya hatari iliyowekwa kulinda mji mkuu dhidi ya mashambulizi ambayo yangefanywa na waasi.

Yevgeny Prigozhin, mkuu wa mamluki wa WagnerPicha: Wagner Group/Zuma/IMAGO

Hata hivyo, Rais Putin mwenyewe hajaonekana hadharani tangu mwisho wa uasi huo, naye Progozhin alionekana mara ya mwisho siku ya Jumamosi wakati msafara wa kundi lake lenye silaha Wagner ulipokuwa ukiondoka katika mji wa kusini mwa nchi hiyo Rostov-on-Don.

Meya wa Moscow asema utulivu umerejea

Meya wa mji mkuu Moscow Sergei Sobyanin alitangaza kwamba hali sasa ni tulivu na aliwashukuru wakaazi wa mji wake kwa kuwa watulivu na wenye uelewa wakati hali ilikuwa ya taharuki.

Viongozi wa kijeshi wa Ukraine hata hivyo wamesisitiza kuwa wanasonga mbele katika nyanja mbalimbali dhidi ya ngome za vikosi vya Urusi kusini na mashariki mwa nchi hiyo.

Putin anusurika na uasi wa kundi la Wagner

Mnamo Jumamosi, wakati mamluki wa Wagner waliposema wanaelekea mji mkuu kuushambulia, huku wakipambana na vikosi rasmi eneo linalopakana na Ukraine, serikali ya Urusi iliamuru kile ilichokiita ‘sheria ya kupambana na ugaidi'.

Uasi huo ulikamilika baada ya saa kadhaa pale Urusi ilipotangaza kuwa makubaliano yamefikiwa kati ya rais wa Belarus na Prigozhin kwamba Prigozhin aende uhamishoni nchini mwake na kwamba wapiganaji wake watasamehewa. Kufuatia makubaliano hayo waliacha lengo lao la kufika Moscow kwa mashambulizi.

Kundi la Wagnener lililenga kupindua uongozi wa jeshi rasmi la UrusiPicha: Russian Defence Ministry/dpa/picture-alliance

Ukraine yadai kukomboa maeneo kadhaa yaliyokamatwa na vikosi vya Urusi

Naibu Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Ganna Malyar amesema vikosi vyao vimekomboa kilomita mraba 17 katika muda wa wiki moja iliyopita hivyo kwa ujumla wameshakomboa 130 kilomita mraba.

Kufuatia uasi wa mamluki wa Wagner na operesheni ya Urusi nchini Ukraine, nchi za Magharibi zinazoiunga mkono Ukraine zinahoji kuwa udhibiti wa madaraka wa Putin umeyumbishwa. 

Mkuu wa Wagner asema wapiganaji wake wameingia Urusi

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borell alifungua mkutano wa mawaziri wa nje wa umoja huo nchini Luxembourg kwa kusema mzozo huo umedhoofisha mamlaka ya Kremlin. Na kwamba yaliyofanyika mwishoni mwa wiki yanaonesha kuwa vita vya Urusi nchini Ukraine vimesababisha mianya katika mamlaka hiyo na vinaathiri mfumo wake wa kisiasa.

(Chanzo: AFPE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW