Urusi yapata pigo baada ya washirika wake kuuawa
2 Machi 2026
Katika kipindi cha miezi 18 iliyopita,rais wa Urusi Vladimir Putin amewapoteza washirika wake wakuu na ameshindwa jinsi ya kuyasaidia mataifa yanahohitaji msaada wake baada ya kutuma vikosi vyake katika mzozo wake na Ukraine.
Tehran kwa muda mrefu,imesimama kama mmoja wa waungaji mkono wa karibu zaidi wa Urusi katika kipindi chote cha mashambulizi ya miaka minne ya Moscow, na Kremlin hapo awali ilitoa wito wa kujizuia kufuatia taarifa za hatua za kijeshi za Marekani zilizokuwa zimekaribia kuchukuliwa dhidi ya Iran.
Mnamo Januari, Rais wa Marekani Donald Trump aliagiza shambulio ambalo vikosi vya Marekani vilimteka kiongozi wa mrengo wa kushoto wa Venezuela, Nicholas Maduro. Washington pia inashirikiana na viongozi wapya wa Syria tangu kuanguka kwa Bashar al-Assad mwishoni mwa mwaka 2024 jambo ambalo lilipunguza pakubwa ushawishi wa Urusi katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa mshauri mwandamizi katika kituo cha Carnegie Russia Eurasia, Alexander Baunov,rais wa Urusi Vladimir Putin yuko katika wakati mgumu kwa sasa.
Ukraine yasema Urusi imeanza kupoteza ushawishi wake
Tangu vita vya Iran na Marekani kuzuka siku ya Jumamosi na kupelekea vifo vya wakuu wa serikali ya Iran, serikali ya Moscow imetuma tu salamu za pole kwa rais wa Iran Masoud Pekeshkian na kutaja mauaji yaliyotokea kama ukiukaji wa wazi wa kanuni za maadili ya kibinadamu na sheria za kimataifa. Hata hivyo,Urusi haijatangaza rasmi msaada wowote wa moja kwa moja kwa Tehran.
Mbunge wa Urusi Anatoly Wasserman, aliiambia gazeti la MK.ru kwamba, katika muda mfupi, vita hivyo vinaweza kuisaidia Urusi endapo vitaongeza bei za mafuta jambo litakaloongeza mapato muhimu ya serikali yanayofadhili uvamizi wake wa Ukraine.
Kwa upande mwingine,Ukraine, ambayo imekuwa ikiishutumu mara kwa mara Iran kwa kuiuzia Urusi silaha ikiwemo ndege za Shahed na makombora ya masafa mafupi, ilisherehekea kile ilichosema kuwa ishara ya kupungua kwa ushawishi wa Urusi.
Waziri wa Mambo ya nje wa Ukraine Andriy Sybiga alisema,Urusi si mshirika wa kuaminika hata kwa wale wanaoitegemea sana.