1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yapeleka silaha za nyuklia za kimkakati nchini Belarus

Daniel Gakuba
26 Mei 2023

Rais wa Belarus Alexander Lukashenko amesema Urusi tayari imeanza kupeleka silaha za nyuklia za kimkakati nchini Belarus, baada ya viongozi wa nchi hizo mbili kutia saini makubaliano juu ya silaha hizo jana Alhamisi.

Russland 9K720 Iskander-M  Kurzstrecken Rakete
Picha: Russian Defence Ministry/TASS

Akithibitisha kupelekwa kwa silaha hizo za nyuklia nchini mwake, Rais wa Belarus Alexander Lukashenko amesema uamuzi juu ya idadi ya silaha hizo na mahali zitakapowekwa umekwishaafikiwa, bila kutoa maelezo ya ziada.

Soma zaidi: Urusi na Belarus zasaini makubaliano ya silaha

Alipoulizwa na mwandishi wa habari iwapo makubaliano yaliyosainiwa jana baina yake na Putin yalikuwa juu ya kile ambacho tayari kipo, Lukanshenko amejibu,

''Ndio, uamuzi ulichukuliwa kujengea juu ya kilichosemwa kwa mdomo. Tulitakiwa kutayarisha mahali pa kuzihifadhi silaha hizo na zana nyingine nchini Belarus. Hayo yote yalifanyika, ndio sababu zoezi la kuhamishwa vichwa vya makombora ya nyuklia limeanza.''

Ingawa Lukashenko hakubainisha zitakapowekwa silaha hizo, taarifa za awali zinasema zitapelekwa karibu ya mpaka na Poland.

Rais Vladimir Putin wa Urusi (kushoto) na mshirika wake wa karibu, Rais wa Belarus Alexander Lukasenko ambao wamesaini makubaliano juu ya silaha za nyukliaPicha: Sergei Karpukhin/TASS/dpa/picture alliance

Medvedev asema Urusi haitajadili na serikali ya Zelenskiy

Katika taarifa nyingine juu ya mzozo wa Ukraine, mwanasiasa wa Urusi anayemuunga mkono kwa dhati Rais Vladimir Putin, Dmitry Medvedev amependekeza njia tatu za kusuluhisha mgogoro uliopo kati ya Urusi na Ukraine, akisema kwa maoni yake njia bora ni kuivunja Ukraine, aliyoiita taifa linalokufa, katika sehemu mbili, ya mashariki ikimezwa na Urusi, na ile ya magharibi ikienda upande wa Umoja wa Ulaya. Amedai hili ndilo chaguo linaloweza kuhakikisha usalama wa kudumu.

Kupitia wazo alilolinadi katika ukurasa wake wa mtandao wa Telegram, Dmitry Medvedev amesema kila mzozo humalizika kupitia majadiliano na huo ni ukweli usioepukika, akaongeza lakini kuwa wakati wowote utawala wa sasa wa Ukraine utakaposalia madarakani, hilo halitowezekana.

Urusi yaishambulia kwa maroketi hospitali mjini Dnipro

Medvedev amesema ikiwa itatokea kinyume na hilo, na Ukraine ikajiunga na Umoja wa Ulaya au jumuiya ya kujihami ya NATO, kwa mtazamo wako hali hiyo italeta hatari kubwa inayoweza kuishia katika vita vikuu vya tatu.

Soma zaidi: Ukraine yadai imezuia mashambulizi ya droni ya Urusi

Jengo la hospitali katika mji wa Dnipro nchini Ukraine likiungua moto baada ya kushambuliwa kwa maroketi ya Urusi (26.05.2023).Picha: DNIPROPETROVSK REGIONAL MILITARY/REUTERS

Kauli yake hiyo iliyonukuliwa na shirika la habari la Urusi, TASS leo Ijumaa, inajiri wakati Urusi ikikishambulia kwa maroketi kituo cha afya katika mji wa Dnipro uliopo katikati mwa Ukraine. Mtu mmoja ameuawa na wasiopungua 15 wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo, ikiwa ni kwa mujibu wa rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy.

Wakati huo huo Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amemuonya rais Vladimir Putin wa Urusi dhidi ya kuuweka mzozo huu na Ukraine katika mkwamo wa milele katika maeneo yaliyonyakuliwa na Urusi.

Kansela wa Ujerumani amuonya Putin juu ya kuugandisha mzozo

Kupitia maoni yake yaliyochapishwa katika gazeti la Köln-Stadt Anzeiger la hapa Ujerumani, Kansela Olaf Scholz amemtaka Putin kuelewa kuwa suluhisho la kudumu ni lile linalotilia maanani maslahi ya kila upande, na kwamba sharti la kwanza kwa suluhisho hilo ni Urusi kuondoka wanajeshi wake kutoka ardhi ya Ukraine.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa serikali ya Ujerumani amejizuia kutoa tamko juu ya hali ya rasi ya Crimea, akisema si jukumu la Ujerumani kuiamulia Ukraine juu ya namna inavyotaka kusuluhisha mzozo wa mipaka yake.

Vyanzo: dpae,afpe

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW