Urusi yapendekeza azimio kulaani machafuko Syria
16 Desemba 2011Bila ya kutazamiwa, Urusi imependekeza azimio hilo, kulaani mashambulio yanayofanywa na serikali ya Rais Bashar al-Assad na pia makundi ya upinzani. Nchi za magharibi katika Baraza la Usalama, zimekaribisha jitahada hiyo ya Urusi, lakini zimesema, mswada huo hata hivyo unahitaji kufanyiwa mabadiliko.
Wamekosoa kuwa machafuko ya wapinzani wa serikali ya Syria na vitendo vya ukatili vinavyofanywa na serikali hiyo, vimewekwa katika kiwango kimoja. Vile vile, mswada huo haupendekezi vikwazo, kama wanachama wengi katika baraza hilo la usalama wanavyotaka.
Hata hivyo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton amesema, nchi za magharibi zitajaribu kushirikiana na Urusi ili azimio la kwanza la Baraza la Usalama liweze kupitishwa kuhusu ukandamizaji unaoendelea Syria. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa zaidi ya watu 5,000 wameuawa katika machafuko ya nchini humo.