1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yarudi katika mkataba wa kusafirisha nafaka za Ukraine

2 Novemba 2022

Urusi imesema itarudi kwenye makubaliano ya kuruhusu usafirishaji wa nafaka muhimu za Ukraine baada ya kujitoa kwenye mkataba huo wikendi iliyopita, hatua iliyotishia kuzidisha njaa kote ulimwenguni.

Istanbul Getreidefrachter aus Ukraine warten auf Durchfahrt durch Bosporus
Picha: UMIT BEKTAS/REUTERS

Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema mapema Jumatano kwamba imepokea uhakikisho kutoka Ukraine kwamba haitafanya shughuli zozote za kijeshi dhidi yake katika njia ya Bahari Nyeusi.

Kupitia taarifa, jeshi limesema kwa serikali ya shirikisho la Urusi, uhakikisho huo unatosha hivyo watarejea kwenye utekelezaji wa makubaliano ya kusafirisha nafaka za Ukraine, taifa linalokumbwa na vita kufuatia uvamizi wa Urusi.

Urusi yataka Ukraine ichunguzwe kuhusu silaha za kibayolojia

Urusi ilijitoa kwenye makubaliano hayo siku ya Jumamosi, ikisema haiwezi kuhakikisha usalama wa meli zinazopita kwenye Bahari Nyeusi kwa sababu ya shambulizi lililofanywa dhidi ya meli zake. Baadhi ya meli zilizoshambuliwa zilikuwa katika njia ya bahari ya kusafirisha nafaka. Ukraine ilisema hivyo ni visingizio vya uwongo.

Mshauri wa rais wa Ukraine Mykhailo PodolyakPicha: Russian Embassy in Belarus/ITAR-TASS/IMAGO

Mshauri wa rais wa Ukraine Mykhailo Podolyak amesema Urusi imerejea kwenye makubaliano hayo baada ya kugundua kuwa usafirishaji wa nafaka utaendelea hata bila ya ushiriki wao.

Zelensky ataka ulinzi katika usafirishaji nafaka za Ukraine

Kupitia taarifa kwa shirika la habari la Reuters, Podolyak amesema uamuzi huo umeonesha kuwa vitisho vya Urusi vya hujuma na kuzidisha machafuko hufeli kila vinapopata jibu Madhubuti.

Bei ya ngano, maharage aina ya soya, mahindi miongoni mwa nafaka nyingine zilishuka maradufu katika masoko ya ulimwengu kufuatia tangazo hilo, ambalo pia lilipunguza wasiwasi wa watu kutoweza kumudu gharama za vyakula.

Lengo la usafirishaji wa nafaka za Ukraine ni kuongeza bidhaa hizo katika masoko ya ulimwengu ili kupunguza mfumuko wa bei na kuepusha njaa katika mataifa masikini.Picha: Yasin Akgul/AFP

Muda wa makubaliano hayo unamalizika Novemba 19. Mwanadiplomasia mmoja wa Ulaya aliyefahamishwa kuhusu mazungumzo ya nafaka hizo ameliambia Reuters kuwa huenda rais wa Urusi Vladimir Putin atatumia urefushaji wa muda wa makubaliano hayo kujipa nguvu na kutawala mazungumzo katika mkutano wa kilele wa kundi la G20 nchini Indonesia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema kurejeshwa kwa usafirishaji wa nafaka kunaonesha ni kiasi gani nchi zinaweza kunufaika zinaposhirikiana.

Makubaliano ya kusafirisha nafaka hizo yanalenga kuepusha njaa katika mataifa maskini kwa kuongeza ngano, mafuta ya alizeti na mbolea katika masoko ya ulimwengu na kusaidia kudhibiti mfumuko wa bei ya bidhaa.

Muda wa makubaliano ya kusafirisha nafaka za Ukraine unatarajiwa kumalizika Novemba 19.Picha: Metin Aktas/AA/picture alliance

Hayo yakijiri, wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema itamuita balozi wa Uingereza kumkabidhi Ushahidi wa madai yake kwamba Uingereza ilihusika katika shambulizi la meli kwenye Bahari Nyeusi eneo la rasi ya Krimea.

Uingereza yakanusha madai ya kuhujumu mabomba ya gesi

Urusi imedai wataalam wa Uingereza waliisaidia Ukraine kufanya shambulizi kutumia droni dhidi ya msafara wa meli eneo hilo wikendi iliyopita.

Aidha Urusi imeishutumu Uingereza kuhusika katika shambulizi la mwezi Septemba dhidi ya mabomba ya gesi ya Nord Stream. Lakini Urusi haijatoa ushahidi wowote wa madai yao.

(RTRE)