Urusi yasema amani yawezekana Syria
12 Septemba 2013Urusi inapendekeza mpango wa hatua nne kwa marekani kutekeleza azma yake ya kutaka kuziharibu silaha za sumu za Syria.Taarifa hizo zimechapishwa na gazeti moja la mjini Moscow katika wakati ambapo waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov anatazamiwa kukutana leo na mwenzake wa Marekani John Kerry mjini Geneva.Suala hilo litajadiliwa kwa kina katika mkutano huo.
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amenukuliwa akisema bado kuna nafasi ya kupatikana amani nchini Syria na ulimwengu haupaswi kuiacha nafasi hiyo ipite bila kuitumia.Lavrov ametowa kauli hiyo mbele ya wanafunzi huko Kazakhstan kabla ya kuelekea mjini Geneva baadae kwa ajili ya mazungumzo na mwenzake wa Marekani John Kerry kuhusu pendekezo la nchi yake ambalo limemfanya hata rais Obama kulitaka Bunge la nchi yake kuakhirisha zoezi la kura ya kutowa ridhaa ya kushambuliwa Syria.
Lavrov ameridhsishwa na hatua ya Syria ya kuridhia mpango wake wa kuitaka nchi hiyo izisabilie silaha zake za sumu chini ya uangalizi wa Kimataifa.Aidha ameonya kuhusu kuchukuliwa hatua za kijeshi dhidi ya Syria akisema ni jambo litakalozidisha mafuta katika moto ambao tayari unawaka na kulitekeleza eneo zima.
Pingamizi la waasi
Hata hivyo kutoka Syria kwenyewe waasi wamelipinga pendekezo la Urusi kuhusu kuzisalimisha silaha za sumu za utawala wa Assad wakisema utawala huo unabidi kufikishwa mbele ya mahakama ya Kimataifa kuhusiana na shambulio la mwezi uliopita lililofanywa karibu na mji wa Damascus ambako silaha za sumu zilitumika na mamia ya watu waliuwawa.
Jenerali Salim Idrsi ambaye ni kamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la waasi nchini humo amesema silaha za sumu zilikuwa chombo cha uhalifu katika shambulio hilo la Agosti 21 katika mji wa Ghouta.Tamko hilo la waasi linakuja saa chache kabla Kerry kuwasili Geneva kwa ajili mkutano wake na Lavrov.Pamoja na hayo Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Lareunt Fabius amebaini kwamba ripoti ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa katika suala la kutumiwa silaha za sumu nchini Syria huenda ikatolewa siku ya Jumatatu.
Akizungumza na redio moja ya kifaransa waziri huyo ameweka wazi kwamba ripoti hiyo itaeleza kwamba yamefanyika mauaji ya halaiki kwa kutumika silaha za sumu na kwamba ripoti hiyo itabaini chanzo cha shambulio hilo.Wachunguzi hao waliondoka Syria Agosti 31 baada ya kukusanya sampuli za ushahidi utakaowasaidia katika uchunguzi wao kuhusu shambulio la Ghouta.
Msimamo wa Marekani
Marekani na washirika wake ambao ni pamoja na Ufaransa wanasema ni utawala wa rais Bashar al Assad uliofanya shambulio hilo lakini serikali hiyo ya mjini Damascus na mshirika wake Urussi wanalitwika mzigo jeshi la waasi.Wajumbe kutoka nchi tano wanachama wa kudumu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa walikuwa na kikao katika Umoja wa Mataifa juu ya Syria ambacho hakikufikia mwafaka hapo jana.
Mazungumzo ya Geneva kwahivyo yanategemewa kuchukuwa siku mbili au tatu na pia yatajadili juu ya kuzitia msukumo juhudi za kuitishwa mkutano wa amani unaonuiwa kumaliza vita vya Syria.Lavrov na Kerry watakutana pia na Lakhdar Brahimi mjumbe wa Kimataifa kujadiliana kuhusu mapngo wa kuwakutanisha waasi na utawala wa Assad katika meza ya mazungumzo.
Mwandishi Saumu Mwasimba
Mhariri:Mohammed AbdulRahman