1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi iko tayari kuboresha mahusiano yake na Marekani

Angela Mdungu
25 Machi 2019

Urusi imesema iko tayari kuboresha mahusiano yake na Marekani lakini ni jukumu la Marekani kuanza kulifanyia kazi jambo hilo

Finnland Treffen Trump und Putin
Picha: picture-alliance/ZumaPress

Kauli ya Urusi inakuja ikiwa ni muda mfupi tangu uchunguzi uliokuwa na nia ya kubaini iwapo Rais Donald Trump na wasaidizi wake wa uchaguzi kwa kushirikiana na Urusi walihusika kuvuruga  uchaguzi mkuu wa mwaka 2016 uliomuweka madarakani.

Urusi imezungumzia uchunguzi wa Mwendesha mashitaka maalumu Robert Mueller,baada ya ripoti fupi ya Muller iliyotolewa siku ya Jumapili ambapo Mwanasheria mkuu wa Marekani William Barr amesema,hakuna ushahidi wa kiuchunguzi unaoonesha kuwa Rais Trump, kwa namna yeyote alizuia haki isitendeke na kumfanya ashinde urais wa mwaka 2016.

Katika mkutano kwa njia ya simu, Msemaji wa Ikulu ya Urusi Dmitry Peskov amesema Urusi haikuwahi na wala haitawahi kuiingilia Marekani wala nchi nyingine katika mambo yake ya ndani. Muda mfupi kabla ya Rais Donald Trump kuingia madarakani, mashirika ya kiitelijensia ya Marekani yaliwahi kuripoti kwamba, Urusi iliingilia matokeo ya Urais ya nchi hiyo, kwa njia ya Kampeni ya kudukua barua pepe na propaganda za mtandaoni dhumuni likiwa ni kutengeneza chuki ndani ya Marekani.

Akizungumzia juu ya kuimarika kwa uhusiano wa Urusi na Marekani baada ya Ripoti ya Mueller, Peskov amesema Rais Vladmir Putin alikwishaweka wazi nia yake ya kuboresha uhusiano na nchi hiyo akikumbushia mkutano kati ya marais hao uliofanyika nchini Finland mwezi Julai mwaka uliopita.

Mwendesha mashitaka maalumu wa Marekani, Robert MuellerPicha: picture-alliance/AP Photo/C. Owen

Uchunguzi huo ulioongozwa na muendesha mashitaka Robert Mueller, uliowahusisha watu 34 wakiwemo wasaidizi na washauri wa Trump, umekamilika ikiwa ni miezi 22 tangu ulipoanza kwa lengo la kubaini iwapo Rais Trump alishirikiana na Urusi kuingilia uchaguzi mkuu wa Marekani wa mwaka 2016, ambao matokeo yake yalimuweka madarakani. Watu 25 kati ya waliokuwa pia wakichunguzwa kuingilia uchaguzi huo ni raia wa Urusi.

Maafisa wa Urusi kwa miezi kadhaa iliyopita walikuwa wakiutazama uchunguzi wa Mueller kama jaribio la kumsaka mchawi dhidi ya Trump ili kuchochea chuki dhidi ya Urusi ndani ya Marekani. Pamoja na kwamba hakuna ushahidi unaomuunganisha Rais huyo wa Marekani moja kwa moja na tuhuma za kuvuruga uchaguzi, uchunguzi huo haujaweka wazi kwamba hakufanya makosa. Kumalizika kwa uchunguzi huo, kumeibua hisia kwamba RaisTrump sasa atakuwa huru kukuza uhusiano wake na Urusi.

Mwandishi:Angela Mdungu/APE

Mhariri: Sekione Kitojo