1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUrusi

Urusi yasema Biden amedhamiria kurefusha vita vya Ukraine

20 Novemba 2024

Kremlin imeutuhumu utawala unaoondoka madarakani wa Rais Joe Biden kwamba unafanya kila unachoweza kurefusha vita vya Ukraine baada ya ripoti kuwa Washington imeidhinisha Ukraine ipatiwe mabomu ya kutegwa ardhini.

Urusi | Dmitry Peskov
Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry PeskovPicha: Mikhail Tereshchenko/TASS/dpa/picture alliance

Ikulu ya Urusi, Kremlin, leo imeutuhumu utawala unaoondoka madarakani wa rais Joe Biden wa Marekani kwamba unafanya kila unachoweza kurefusha vita vya Ukraine baada ya ripoti kuwa Washington imeidhinisha Ukraine ipatiwe mabomu ya kutegwa ardhini.

Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, amewaambia waandishi habari mjini Moscow kuwa yeyote anayefuatilia kinachofanywa na utawala wa Marekani atabaini dhamira ya Washington ya kuvirefusha vita vya Ukraine.

Soma pia: Urusi ina imani ndogo kuwa Trump ataumaliza mzozo wa Ukraine 

Matamshi hayo ya Peskov yanafuatia taarifa kwamba Rais Biden ametoa idhini ya kuipatia Ukraine mabomu zaidi ya kutegwa ardhini ili kupunguza kasi ya kusonga mbele kwa vikosi vya Urusi. Uamuzi huo umekosolewa vikali na asasi ya kimataifa inayopinga matumizi ya mabomu ya kutegwa ardhini kwenye mizozo duniani.

Marekani tayari ilikwishatoa ruhusa kwa Ukraine kutumia makombora yake ya masafa ya kati kuyashambulia maeneo ya ndani ya Urusi, hatua ambayo ilikosolewa vikali na viongozi mjini Moscow.