1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yasema watu 126 wameondolewa Mariupol

2 Mei 2022

Jeshi la Urusi limesema watu 126 hadi sasa wameondolewa kutoka kwenye kiwanda cha chuma cha Azovstal kilichozingirwa kwenye mji wa Mariupol na kupelekwa sehemu salama.

Ukraine | Krieg | Evakuierung aus Mariupol
Picha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Urusi imeeleza leo kuwa zaidi ya nusu ya watu walioondolewa kuanzia siku ya Jumamosi walichagua kupelekwa kwenye eneo linalodhibitiwa na Ukraine. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, raia 69 walioamua kuondoa kwenye eneo linalotawaliwa na Ukraine wamekabidhiwa kwa wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na Shirika la Msalaba Mwekundu na kwa sasa wanaelekea Zaporizhzhia katika msafara wa magari.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa jeshi la Urusi limewahakikishia usalama wao katika njia zilizoachwa wazi kwa ajili ya masuala ya kiutu. Jana Rais wa Ukraine, Volodmyr Zelensky alisema takribani raia 100 waliokuwa wamekwama kwenye kiwanda hicho waliondolewa na wamewasili leo Zaporizhzhia.

Walinzi wa taifa wa Ukraine wamesema raia 200 bado wamekwama kwenye kiwanda hicho, wakiwemo watoto 20. Aidha, baadhi ya wapiganaji 500 wa Ukraine bado wako kwenye kiwanda hicho na wanahitaji haraka msaada wa matibabu.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi, Meja Jenerali Igor Konashenkov Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Zemlianichenko

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi, Meja Jenerali Igor Konashenkov pia ametangaza Jumatatu kuwa mashambulizi mapya ya anga na mashambulizi ya makombora yamefanyika dhidi ya Ukraine. ''Kikosi cha anga na marubani wa kijeshi wameyashambulia maeneo 27 waliyoyalenga. Makombora yamevishambulia vituo 38 vya kijeshi vya Ukraine. Pia mfumo mmoja wa kujikinga na makombora wa Osa AKM na mzinga wenye maroketi kadhaa yameharibiwa karibu na Arkhanhelivka,'' alifafanua Konashenkov.

Israel na Ukraine zakosoa matamshi ya Lavrov

Huku hayo yakijiri, viongozi wa Israel na Ukraine wamemkosoa Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov kwa kumlinganisha aliyekuwa dikteta wa Ujerumani Adolf Hitler na Rais Volodmyr Zelensky, wakisema kuwa sio sahihi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba amesema Lavrov hakuweza kuficha chuki iliyokita mizizi dhidi ya Wayahudi. Amesema matamshi hayo ni dharau kwa Zelensky, Ukraine, Israel na Wayahudi. Lavrov alisema Jumapili kuwa Zelensky anaweza kuwa Myahudi, lakini Hitler pia alikuwa na vinasaba vya Kiyahudi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro KulebaPicha: Evelyn Hockstein/AP/picture alliance

Ama kwa upande mwingine, Marekani ina matumaini kwamba wanadiplomasia wake watarejea Kiev ambako nchi hiyo iliufunga ubalozi wake siku chache kabla ya uvamizi wa Urusi, ifikapo mwishoni mwa mwezi huu. Akizungumza katika mji wa magharibi wa Lviv, Kristina Kvien anayehusika na masuala ya kibalozi amesema leo kuwa wana imani mazingira yataruhusu kurejea Kiev.

Ulaya kuwasilisha awamu mpya ya vikwazo kwa Urusi 

Wakati huo huo, Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya inatarajiwa kuwasilisha awamu mpya ya vikwazo kwa urusi siku ya Jumatano. Maafisa wa umoja huo wamesema leo mjini Brussels kuwa pendekezo la awamu ya sita ya vikwazo huenda vikajumuisha marufuku ya mafuta pamoja na hatua zaidi za kuchukua za adhabu dhidi ya watu binafsi na makampuni ya Urusi.

Nao Umoja wa Mataifa umesema kuwa idadi ya raia waliouawa nchini Ukraine tangu Urusi ilipoivamia nchi hiyo Februari 24, imezidi 3,000. Ofisi ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR imesema Jumatatu mjini Geneva kwamba wengi wa raia hao waliuawa kwa mashambulizi ya makombora ya ardhini na yaliyofyatuliwa na ndege za kivita.

(AFP, DPA, AP, Reuters)