Mashambulizi yafanyika Urusi na Ukraine
13 Septemba 2023Watu 24 wamejeruhiwa na meli mbili zilizokuwa zinafanyiwa matengenezo ziliharibiwa katika shambulio la Ukraine kwenye mji wa bandari wa Sevastopol ambao hutumika kama bandari kuu ambako meli za Urusi huwa zinaegesha katika Bahari Nyeusi. Kwenye shambulio hilo maafisa wa Urusi wamesema moto ulizuka katika eneo la bandari lililoshambuliwa. Ukraine ilifanya mashambulizi wakati Urusi ilipoanzisha mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kuelekea mkoa wa Odesa wa kusini mwa Ukraine.
Gavana wa jimbo la Odessa, Oleh Kiper amesema mashambulio hayo ya Urusi yameharibu bandari na miundombinu ya kiraia katika wilaya ya Izmail ambayo haiko mbali na jiji la Crimea. Gavana huyo amesema watu saba walijeruhiwa. Jeshi la anga la Ukraine limesema limefanikiwa kunasa ndege 32 zisizo na rubani aina ya Shahed kati ya ndege 44 zilizotumiwa na Urusi ambazo nyingi zilielekezwa katika sehemu za kusini za mkoa wa Odessa.
Soma:Marekani kuipatia Ukraine makombora ya masafa marefu
Rasi ya Crimea, ambayo Urusi ilitwaa kutoka Ukraine mnamo mwaka 2014 katika kitendo ambachokililaaniwa na jamii ya kimataifa, imekuwa mara kwa mara inalengwa na mashambulizi tangu Rais wa Urusi Vladimir Putin alipoamuru uvamizi wa Ukraine zaidi ya miezi 18 iliyopita.
Wakati huo huo Romania nchi mwanachama wa NATO imesema imevipata vipande vipya vya ndege zisizo na rubani karibu na mpaka wake na Ukraine. Wizara ya Ulinzi ya Romania kwenye tamko lake imesema kumekuwepo na matokeo matatu kama hayo katika wiki iliyopita.
Romania imesema helikopta mbili za jeshi la wanahewa zilipelekwa pamoja na wataalamu kwenye miji ya Nufaru na Victoria katika kaunti ya mashariki ya Tulcea ambako vipande vinavyoaminika kuwa ni vya ndege zisizo na rubani vimeenea katika eneo la mita kadhaa.
Soma:Putin: Operesheni ya Ukraine haijapata mafanikio
Wizara ya ulinzi ya Romania imesema imeijulisha idara ya Ukaguzi wa Hali za Dharura kuhusu maeneo ya karibu na mpaka ambayo yanaweza kuwa katika hatari ikiwa vikosi vya Urusi vitazishambulia bandari za Ukraine zilizoko katika mto Danube kutokea upande wa pili wa Romania.
Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine Oleksandr Kubrakov amesema kiwango cha kupeleka nje nafaka kutokea bandari za Ukraine katika mto Danube kimepungua kwa karibu tani milioni 0.5 kwa mwezi kwa sababu ya mashambulizi ya Urusi.
Vyanzo:AP/RTRE
Mhariri: