1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yashambulia hospitali tatu Ukraine

10 Machi 2022

Mamlaka nchini Ukraine zinasema ndege za Urusi zimezishambulia hospitali tatu usiku wa kuamkia Alkhamis (Machi 10) magharibi mwa mji mkuu, Kyiv, na kwenye mji wa bandari wa Mariupol, huku juhudi za uokozi zikiendelea.

Ukraine zerstörte Geburtsklinik in Mariupol
Picha: Evgeniy Maloletka/AP/picture alliance

Mashambulizi hayo yamekuja kukiwa na matumaini ya kuwahamisha raia kutoka miji kadhaa iliyozingirwa, ukiwemo Mariupol, ambao hauna chakula, maji, wala umeme kwa siku kadhaa sasa.

Mji huo umezingirwa na majeshi ya Urusi kwa siku tisa sasa, huku maafisa wa mji wakisema kuwa wakaazi wake 1,200 wameshauawa na wafanyakazi wa kujitolea wameanza kuzizika maiti kwenye makaburi ya pamoja kutokana na kujaa kwa maeneo ya kuzikia.

Mkuu wa mkoa wa Kyiv, Oleksiy Kuleba, alisema kupitia televisheni kwamba "jeshi la Urusi limeyageuza maisha kuwa jahanamu, ambapo watu wanajificha chini ya mahandaki mchana na usiku wakiwa hawana chakula, maji wala umeme."

Mji mwengine ulioshambuliwa vikali kwa mabomu ni Zhytomyr wenye wakaazi 260,000 na ulio magharibi mwa mji mkuu, Kyiv. Meya wa mji huo, Serhii Sukholym, alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook kwamba "hospitali mbili zilmeshambuliwa, mojawapo ikiwa ya watoto." 

Mjamzito aliyejeruhiwa akishuka ngazi kwenye jengo la hospitali iliyoshambuliwa mjini Mariupol.Picha: Evgeniy Maloletka/AP/picture alliance

Katika mji wa pili kwa ukubwa, Kharkiv, makombora ya Urusi yaliharibu makao makuu ya polisi, na kuwauwa watu wanne na kuwajeruhi wengine 15, kwa mujibu wa mwakilishi wa ofisi ya mwendesha mashitaka, Serhii Bolvinov, ambaye aliongeza kuwa tangu uvamizi kuanza wiki mbili zilizopita, wakaazi 282 wa mji huo wameshauawa, sita kati yao wakiwa watoto wadogo.

Zelenskyy azidi kuomba msaada wa Magharibi

Kwenye hotuba yake ya kila siku, Rais Volodymr Zelenskyy alisema juhudi zinaendelea kuwaokowa watu 18,000 waliokwama kwenye mkoa wa Kyiv, akiongeza kuwa kufikia Jumatano jioni, watu 35,000 walishakimbilia maeneo salama kupitia njia zilizowekwa kuwaokowa.

Operesheni za kuwahamisha raia zilitazamiwa kuendelea kwenye maeneo mengine kadhaa, ukiwemo mji wa kaskazini mashariki wa Sumy, ambako watu 5,000 walihamishwa siku Jumanne. 

Rais Volodymyr Zelensky akitoa hotuba yake ya kila siku, usiku wa Jumatano ya Machi 9,2022 mjini Kyiv.Picha: AFP

Rais Zelenskyy aliyataka mataifa ya Magharibi kuzidisha vikwazo vikali zaidi dhidi ya Urusi, baada ya mashambulizi ya anga dhidi ya hospitali ya wazazi kwenye mji wa Mariupol usiku wa kuamkia leo, ambapo watu 17 walijeruhiwa, wakiwemo wajawazito.

Zelenskyy alisema "mauaji ya maangamizi dhidi ya watu wa Ukaine yanafanyika na ni wajibu wa mataifa ya Magharibi kuimarisha vikwazo ili Urusi isiweze tena kuendelea na mauaji hayo."

Kwa mara nyengine, Zelenskyy aliyataka mataifa ya Magharibi kuweka marufuku ya ndege kuruka kwenye anga la Ukraine, ombi ambalo wanachama wa muungano wa kijeshi wa NATO wamelikataa mara kadhaa kwa khofu kwamba hatua hiyo itasababisha vita vya moja kwa moja na Urusi, ambavyo wanavikwepa. 

Kwa kushindikana hilo, Zelenskyy aliomba ndege zaidi za kivita kwa ajili ya nchi yake, pendekezo ambalo pia lilikataliwa na wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, hapo jana Jumaatano. 

Awali, Poland ilisema ingelikabidhi ndege zake chapa MiG-29 kwa NATO kwa ajili ya kulisaidia jeshi la Ukraine, lakini msemaji wa Pentagon, John Kirby, aliwaambia waandishi wa habari kwamba Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin alizungumza na mwenzake wa Poland na kumueleza kuwa "hatua hiyo ni ya hatari na pia haitabadilisha chochote kwenye uwezo wa jeshi la anga la Ukraine."

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW