Urusi yashambulia kwa droni kaskazini mwa Ukraine
12 Septemba 2024Watu 14 wamejeruhiwa kwenye mashambulizi hayo ya usiku kucha na ambayo yamesababisha kukatika kwa umeme kwenye makazi.
Kwa mujibu wa viongozi wa eneo hilo kumekuwepo na milipuko 10 wakati wa shambulio hilo. Meya wa mji huo wa Konotop, Artem Semenikhin amesema mfumo wa nguvu za umeme umeharibiwa vibaya.
Mji huo uko katika eneo la Sumy, ambalo limekuwa likilengwa na mashambulizi ya Urusi katika wiki za hivi karibuni.
Mafundi wanaendelea na utaratibu wa kurejesha nguvu za umeme katika mji huo, ambao ulikuwa na wakazi wapatao 83,000 kabla ya vita.
Kulingana na jeshi la anga la Ukraine, mashambulizi katika mji wa Konotop yalihusisha ndege zisizo na rubani 64 zilizovurumishwa na Urusi, lakini wanajeshi wa Ukraine walifanikiwa kuzidungua droni 44 kati ya hizo zilizolenga zaidi ya mikoa tisa.
Inaarifiwa kuwa shambulio hilo pia liliharibu majengo saba ya ghorofa, taasisi za matibabu na elimu, maduka, benki na sehemu ya njia ya usafiri wa treni.
Soma pia: Urusi yakisahambulia kwa droni kituo cha nishati cha Sumy
Ukraine iliitumia Sumy kama eneo la kufanya mashambulizi ya kushtukiza kuvuka mpaka kuingia Urusi mwezi uliopita kwa nia ya kujaribu kuchukua udhibiti katika uwanja wa vita wakati vikosi vya Urusi vikisonga mbele mashariki mwa Ukraine.
Ingawa Ukraine inakabiliwa na uhaba mkubwa wa risasi na makombora ya masafa marefu, imeendelea kujaribu kuvirudisha nyuma vikosi vya Urusi kwa kuzindua mashambulizi ya mamia ya ndege zisizo na rubani.
Uungwaji mkono Ukraine hautapungua
Huku haya yakijiri, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amewasili nchini Poland ambako atakutana na Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk, Rais Andrzej Duda na Waziri wa Mambo ya Nje Radoslaw Sikorski, ili kujadili uungaji mkono kwa Ukraine katika vita vyake dhidi ya Urusi na kuimarisha ushirikiano wa ulinzi kati ya Marekani na Warsaw.
Ziara ya Blinken inajiri siku moja baada ya Marekani na Uingereza kuahidi kutoa karibu dola bilioni 1.5 kusaidia Ukraine.
Soma pia: Mawaziri Blinken na Lammy waapa kuisaidia zaidi Ukraine
Blinken alisema "Ujumbe wetu wa pamoja kwa Putin uko wazi, Uungwaji mkono wetu hautapungua, umoja wetu hautavunjika. Putin hataupita muungano wa nchi zilizojitolea kwa mafanikio ya Ukraine, na hakika hatawashinda watu wa Ukraine."
Aidha Marekani na Uingereza zimeahidi jibu la haraka kwa maombi ya Kyiv ya kupunguza vikwazo vya silaha zinazoweza kutumia kuishambulia zaidi Urusi.
Kupitia shirika la habari la TASS, Ikulu ya Kremlin imeonya kwamba kuiruhusu Ukraine kutumia silaha kutoka nchi za Magharibi kuishambulia Urusi, kutaongeza ushiriki wa Magharibi katika kuchochea mzozo huo.