Urusi yashambulia maeneo ya jimbo la Donetsk
14 Februari 2023Ukraine imeripoti mashambulizi ya Urusi yaliyofanywa kwenye maeneo ya mapambano na maeneo 16 ya makaazi karibu na mji wa Bakhmut.
Katika muda wa siku tatu zilizopita, wapiganaji wa kampuni binafsi ya kijeshi ya Urusi ya Wagner wamezidi kusonga mbele kaskazini mwa viunga vya mji wa Bakhmut. Taarifa zinaeleza kuwa maafisa wameanza kuwaondoa raia kwenye maeneo hayo.
Mashambulizi hayo yanafanyika wakati ambapo mawaziri wa ulinzi wa Jumuia ya Kujihami ya NATO wanakutana mjini Brussels kujadiliana kuhusu kongeza silaha kwa Ukraine.
Nchi za Magharibi zatakiwa kupeleka silaha zaidi Ukraine
Mapema leo Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg alizitolea wito nchi za Magharibi kupeleka Ukraine silaha zaidi inazohitaji ili kuvishinda vita vya Urusi.
Naye Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin amesema Ukraine inahitaji haraka silaha katika wakati huu muhimu wa vita. Akizungumza na mawaziri wenzake wa NATO, Austin amesema katika mwaka huu mmoja wa vita, NATO imeendelea kuungana zaidi na kwamba Marekani itaendelea kuisaidia Ukraine.
"Marekani, Ujerumani, Uholanzi zinashirikiana pamoja kuipatia Ukraine mitambo ya kurushia makombora aina ya Patriot. Ufaransa na Italia zinashirikiana kutoa mifumo ya kuzuia makombora aina ya SAMP/T. Na muungano wa nchi, ikiwemo Ujerumani, Poland, Canada, Ureno, Uhispania, Norway, Denmark, na Uholanzi zinashirikiana kuipa Ukraine vifaru chapa Leopard," alisisitiza Austin.
Hata hivyo, ikulu ya Urusi, Kremlin imesema Muungano huo wa Kijeshi wa NATO unaoongozwa na Marekani umekuwa ukijaribu kujiingiza zaidi kwenye mzozo wa Ukraine na kila siku umekuwa ukionesha wazi uadui wake dhidi ya Urusi.
Upelekaji silaha Ukraine kunauzidisha mzozo uliopo
Hayo yameelezwa leo na msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov wakati akizungumza na waandishi habari, ambapo amesema hatua ya nchi wanachama wa NATO kupeleka silaha Ukraine, inauzidisha mzozo uliopo.
Hata hivyo, Ukraine na mataifa ya Magharibi yamekuwa yakisema msaada huo ni kwa ajili ya kuisaidia Ukraine kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Urusi.
Waziri wa Ulinzi wa Norway Bjørn Arild Gram, amesema nchi hiyo itaipatia Ukraine vifaru vinane vinavyotengenezwa Ujerumani chapa Leopard 2 pamoja na vifaa vingine.
Akizungumza katika mkutano wa NATO, Gram amesema Norway pia itapeleka magari manne ya kijeshi pamoja na pesa kwa ajili ya kununulia risasi na vipuri. Norway ambayo inapakana na Urusi katika eneo la Arctic, ina jumla ya vifaru 36 chapa Leopard 2.
(AFP, DPA, Reuters)