Urusi yashambulia miundombinu ya nishati ya Kyiv
27 Novemba 2025
Wizara ya ulinzi ya Urusi imeripoti kwamba katika muda wa saa 24 zilizopita, majeshi ya nchi hiyo yamefanya mashambulizi yaliyolenga miundombinu ya nishati na uchukuzi nchini Ukraine pamoja na viwanda vya kutengeneza risasi katika maeneo 143.
Urusi imeongeza kwamba vikosi vyake vya ulinzi wa anga vimefanikiwa kudungua mabomu sita yanayoongozwa kutoka angani, makombora manne aina ya HIMARS yaliyotengenezwa Marekani na droni 154.
Ama kwa upande mwengine, makao makuu ya jeshi la Ukraine yameeleza kwamba vikosi vya nchi hiyo vimefanya shambulio lililolenga kiwanda cha kimkakati cha kijeshi cha VNIIR-Progress kilichoko eneo la Cheboksary, katikati mwa Urusi. Kiwanda hicho kinatumika kutengeneza sehemu ya silaha za kijeshi ikiwemo droni na makombora.
Ukraine imesema kuwa inafanya tathmini juu ya uharibifu kwenye kiwanda hicho cha silaha.
Warepublican waukosoa mpango wa amani wa Trump
Wakati hayo yakijiri, wabunge kadhaa wa chama cha Republican nchini Marekani wamemkosoa Rais Donald Trump kuhusu jinsi anavyoshughulikia pendekezo la mpango wa amani wa Ukraine, wakisema unainufaisha zaidi Urusi.
Ukosoaji huo ni mabadiliko makubwa kwa mtazamo wa chama ambacho kwa kawaida kimeunga mkono karibu kila hatua ya Trump.
Hali hiyo pia inaonekana kuashiria mgawanyiko ndani ya chama, hasa katika kipindi ambacho vita vya Ukraine vinaendelea kuibua mjadala wa kimataifa kuhusu mustakabali wa amani nchini humo.
Hawa ni baadhi ya waakazi wa Kyiv wakitoa maoni yao kuhusu pendekezo hilo la mpango wa amani.
"Trump ni mtu anayefanya kila kitu kwa manufaa ya Putin. Hafikirii kuhusu Ukraine kabisa. Ni mfano wa mtu kuingia nyumbani kwako, na kuchukua nusu ya vitu vyako, na kukusukuma kwenye chumba cha kuhifadhia vitu, na kukuambia ukae pale."
"Hii ni kujisalimisha kwa amani tu lakini kwa kweli, natamani sana haya yote yaishe, kwa sababu ni janga. Baba wa rafiki yangu amekufa hivi karibuni katika uwanja wa vita. Sitaki mtu mwingine yeyote ahisi maumivu haya."
Waungaji mkono wa Ukraine wameonyesha wasiwasi kwamba mpango huo wa amani wenye mapendekezo 28 uliotayarishwa na Marekani kwa ajili ya kumaliza vita nchini Ukraine, na ulioripotiwa kwa mara ya kwanza wiki iliyopita, unamaanisha kuwa serikali ya Trump inaweza kuwa tayari kuishinikiza Kyiv kusaini makubaliano ya amani yanayoipendelea Moscow.
Seneta Roger Wicker ambaye ni mwenyekiti wa Republican wa Kamati ya Seneti ya Huduma za Kijeshi, alisema katika taarifa mnamo siku ya Ijumaa, "Mpango huu unaoitwa mpango wa amani una matatizo makubwa, na nina mashaka iwapo utaweza kuleta amani."
Wasiwasi juu ya mpango huo wa amani uliongezeka baada ya shirika la Habari la Bloomberg News kuripoti siku ya Jumanne kwamba mjumbe wa Trump, Steve Witkoff, katika mazungumzo ya simu na mshauri wa sera wa Rais wa Urusi Vladimir Putin, Yuri Ushakov, alisema kwamba wanapaswa kushirikiana katika mpango wa kusitisha mapigano na kwamba Putin anapaswa kulijadili suala hilo na Trump.
Naye mwakilishi wa Republican Don Bacon ameandika katika mtandao wa kijamii wa X, "Kwa wale wanaopinga uvamizi wa Urusi na wangependa kuiona Ukraine ikipata ushindi na kuwa nchi huru na ya kidemokrasia, ni wazi kwamba Witkoff anaiunga mkono Urusi kikamilifu na kwamba hawezi kuaminika kuongoza mazungumzo haya."
Ingawa chama cha Trump bado kinamuunga mkono kwa kiasi kikubwa, ukosoaji kutoka kwa wabunge wa Republican sio wa kupuuzwa hasa kutokana na misukosuko ya hivi karibuni ndani ya chama, ikiwemo ushindi wa Democrats katika chaguzi za mwezi huu na hatua ya bunge la Congress kuidhinisha kutolewa kwa mafaili ya Idara ya Haki kuhusu Jeffrey Epstein, mhalifu wa kingono aliyewahi kutiwa hatiani.