Urusi yashinikizwa na NATO kundosha vikosi vyake Georgia
19 Agosti 2008Kwenye mkutano huo wa dharura ulioitishwa na Marekani,mawaziri wa mambo ya nje wa NATO wameiunga mkono Georgia na wameitaka Urusi iondoshe vikosi vyake kutoka Georgia.Mawaziri hao wa nchi 26 wanachama wa jumuiya ya kujihami ya nchi za magharibi-NATO wamekubali kuwa hawatoweza kuendelea na shughuli zao na Urusi kama kawaida,il hali vikosi vyake vipo Georgia.
Wamesema,NATO inazingatia kwa dhati vipi vitendo vya Urusi vitaathiri uhusiano wa pande hizo mbili huku Marekani ikitoa wito wa kuchunguza kikamilifu uhusiano wa NATO na Moscow.Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Condoleezza Rice amesema,Urusi inajitenganisha na maadili ya ushirikiano katika jumuiya ya mataifa kwa yale yanayotendwa wakati wa mzozo wa hivi sasa nchini Georgia. Lakini akaongezea:
"Marekani haitaki kuitenga Urusi.Ni Marekani iliyokuwa na mfumo wa mkakati wa ushirikiano pamoja na Urusi-kuanzia ushirikiano wa kiuchumi,kisiasa,kitamaduni na ipo tayari pia kushirikiana upande wa ulinzi."
Kwa upande mwingine,Katibu Mkuu wa NATO,Jaap de Hoop Scheffer alipozungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Brussels,alisisitiza kuwa hivi sasa Urusi haiheshimu mpango wa amani uliokubaliwa pamoja na Rais Dmitry Medvedev.Kwa hivyo mustakabali wa uhusiano wa NATO na Urusi utategemea hatua madhubuti zitakazochukuliwa na nchi hiyo kutekeleza yale yaliyokubaliwa-yaani kuondoa majeshi yake kutoka Georgia.
Hata mawaziri wa NATO,katika taarifa ya pamoja iliyotolewa mwishoni mwa kikao hicho cha dharura,wametoa wito kwa Urusi kuonyesha kwa maneno na vitendo kuwa inaendelea kuwajibika kwa maadili ya msingi wa uhusiano wao.Wamezilaani hatua za kijeshi zilizochukuliwa na Urusi nchini Georgia na kusema kuwa zilipindukia kiasi na wala haziambatani na dhima yake ya kulinda amani.Mawaziri wengi wamesisitiza umuhimu uliopo kwa Urusi kuheshimu masharti ya makubaliano ya kusitisha mapigano,yaliotiwa saini pamoja na Georgia.Wameikumbusha Moscow wajibu wa kuhifadhi usalama na utulivu katika maeneo yalio chini ya udhibiti wake,hasa wakati huu ripoti zikiendelea kusema kuwa majeshi ya Urusi makusudi yanateketeza mali za raia.
Kwa upande wake,jeshi la Urusi limesema linachelewesha kuondosha vikosi vyake kutoka Georgia kwa sababu linataka kuzuia pengo la mamlaka litakalosababisha machafuko zaidi kaskazini mwa nchi.