1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yashukiwa kumpa sumu aliyekuwa jasusi wake

6 Machi 2018

Uingereza yaapa kuchukua hatua kali dhidi ya nchi yoyote itakayothibitika kuhusika na tukio la kumdhuru mtu anayetajwa kuwa jasusi wa zamani wa Urusi

Video-Still Sergej Skripal, ehemaliger Oberst des russischen GRU-Militärgeheimdienstes
Sergei SkripalPicha: Reuters TV/RTR

Polisi ya Uingereza iko katika harakati za kufanya uchunguzi wa kutambua kitu kisichojulikana kilichosababisha aliyekuwa jasusi wa Urusi kuwa katika hali mahututi baada ya kuugua ghafla na  kuanguka. Mbunge mmoja wa ngazi ya juu Uingereza amedokeza kwamba huenda Urusi ina mkono wake katika shambulizi hilo dhidi ya   Sergei Skripal.

Urusi inashukiwa kuwa nyuma ya tukio hilo ambapo waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Jonson ameliambia bunge kwamba Uingereza itachukua hatua mwafaka na kubwa ikiwa itathibitisha kwamba kuna serikali iliyohusika katika tukio hilo ambalo amelitaja kuwa tukio linalosumbua huku akikumbushia kisa cha kuuwawa aliyekuwa jasusi wa Urusi Alexander Ltvinenko mwaka 2006. Lakini Serikali mjini Moscow imeshasema haina taarifa yoyote kuhusu mkasa wa kuanguka na kupoteza fahamu uliomfika mtu  aliyetambuliwa na vyombo vya habari kwa jina la Sergei Skripal huko kusini mwa Uingereza katika mji unaoitwa Salisbury siku ya Jumapili lakini msemaji wa rais Putin Dmitry Peskov anasema Urusi  itafurahi sana kutoa ushirikiano ikiwa maaofisa wa Uingereza watatoa ombi hilo.

''Kwa bahati mbaya siwezi kuwapa maoni yoyote kuhusu kisa cha Sergei Skripal,kwasababu hatuna taarifa yoyote.Mnaelewa  ni jinsi gani alivyoishia Magharibi kutokana na matokea ya hatua zipi na maamuzi gani- Sitorudia kuzungumzia mambo haya.Sasa tunaona kilichotokea lakini pamoja na hilo sisi hatuna taarifa yoyote kuhusu kitu gani ambacho huenda kimesbabisha tukio hilo na pia hatufahamu nini hasa mtu huyu alikuwa akikifanya maishani mwake hivi karibuni.''

Alexander Litvinenko aliuwawa kwa sumu na Urusi mjini London 2006Picha: Getty Images/AFP/M. Hayhow

Maafisa wataalaamu kutoka kitengo cha kupambana na ugaidi wanajaribu kusaidia katika uchunguzi wa tukio hilo ambalo pia limesababisha mwanamke mmoja wa umri wa miaka 33 ambaye anatajwa kuwa ni bintiyake Skripal kuwa katika hali mahututi katika kile ambacho kinakhofiwa kuwa ilikuwa ni njama ya kuwapa sumu. Skripal mwenye umri wa miaka 66 aliwahi kuwa kanali katika kitengo cha ujasusi katika jeshi la Urusi naye pia yuko katika hali mahututi kwenye hospitali ya wilaya ya Salisbury. Polisi haijathibitisha majina yao lakini imethibitisha kwamba watu wawili wenye umri wa miaka 66 na 33 wanatibiwa katika hospitali hiyo kutokana na kuwa katika mazingira  yaliyokuwa na sumu ambayo haifahamiki.

Pia polisi imedokeza kwamba mtu mmoja kutoka kwenye kitengo cha huduma ya dharura aliyesaidia kukabiliana na tukio hilo pia amelazwa hospitali. Tukio hilo limetajwa kuwa ni  kubwa na eneo zima walikokutikana watu hao lililazimika kufungwa  ili kuzuia watu wasifike hii leo wakati mgahawa ulioko katika na mtaa huo pia nao umefungwa kwajili ya kuchukuwa tahadhari. Tukio hilo linakumbusha mauaji ya jasusi mwingine wa zamani wa Urusi Alexander Litvinenko hukohuko nchini Uingereza.Livinenko alikuwa pia ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Urusi na aliuwawa kwa kulishwa sumu aina ya Polonium  mnamo mwaka 2006 mjini London kwa maelekezo kutoka Urusi. Itakumbukwa kwamba tukio hilo lilisababisha mvutano mkubwa wa kidiplomasia na mpasuko kati ya serikali ya mjini London na Moscow,na kwa maana hioyo kifo kingine ambacho kitaihusisha Urusi nchini Uingereza kinaweza kufufua upya mvutano mkubwa zaidi.

Picha: picture-alliance/dpa/A.Zemlianichenko

Tom Tugendhat mwenyekiti wa kamati ya masuala ya mambo ya nje katika bunge la Uingereza  ameonya kuhusu kule ushahidi unakoelekea akisema kwamba ni mapema mno kusema ikiwa ni kweli au si kweli lakini hapana shaka kila dalili zinaonesha ni shambulio lililofanywa na Urusi.Polisi inaendelea na uchunguzi wake ingawa imesema kwamba hakuna kitisho kinachoukabili umma. Skripal aliwahi kufungwa jela miaka 13 nchini Urusi mwaka 2006 kwa kosa la kuisaliti mashirika ya kijasusi ya Urusi kwa kutowa taarifa kwa idara ya ujasusi ya Uingereza MI6.

Alipata msamaha kabla ya kusafirishwa kwenda Uingereza kama sehemu ya kubadilishana majaasusi wa ngazi ya juu kati ya Urusi na Marekani mwaka 2010. Uchunguzi wa Uingereza mwaka 2016 uliobaini kwamba kuna uwezekano  rais Vladmir Putin aliidhinisha kuuwawa kwake na watu wawili waliotajwa kuwa washukiwa wakuu  ni Andrei Lugovoi na Dmitri Kovtun.Lakini jana msemaji wa Putin Dmitry Peskov alisema kwamba Urusi haina taarifa yoyote kuhusu kisa hicho cha Salisbury.

Mwandishi:Saumu Mwasimba.

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW