Urusi yasikitishwa na Marekani kukataa kuandaa mazungumzo
22 Machi 2021Katika taarifa, wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema kwamba fursa nyingine ya kutafuta suluhisho la uhusiano kati ya Marekani na Urusi imepitwa na kwamba jukumu hilo limo kikamilifu mikononi mwa Marekani. Wiki iliyopita, Putin alipendekeza kuandaliwa kwa mazungumzo kati yake na Biden kwa njia ya video baada ya rais huyo wa Marekani kumtaja kuwa ''Muuaji.''
Alipendekeza mazungumzo hayo yawe ya wazi na ya moja kwa moja na kumtaka Biden kufanya hivyo aidha siku ya Ijumaa ama Jumatatu. Putin aliongeza kuwa mazungumzo hayo yatakuwa ya kuvutia kwa watu wa Urusi na Marekani. Lakini Biden aliwaambia wanahabari kwamba wawili hao watazungumza tu wakati mmoja.
Wakati wa mahojiano na shirika la habari la ABC siku ya Jumatano alipoulizwa iwapo anadhani Putin anayeshutumiwa kwa kuagiza kupewa sumu kwa kiongozi wa upinzani Alexei Navalny Ni ''muuaji'' Biden aliitikia kwa kukubali. Pia alisema kuwa Putin atalipia kwa kujaribu kuhujumu uwaniaji wake wakati wa uchaguzi wa Marekani wa mwaka 2020.
Hata hivyo, akizungumza wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka saba tangu Urusi kuliteka eneo la Crimea, Putin alifutilia mbali uwezekano wa kukatiza uhusiano na Marekani. Akijibu kuhusu matamshi ya Biden ya kumuita muuaji, Putin alisema kuwa huchukuwa mtu kumjuwa mtu na kwamba anamtakia kiongozi huyo afya njema.
Siku ya Alhamisi, Ikulu ya Marekani White House ilisema kuwa Biden hajutii matamshi yake.
Msemaji wa ikulu hiyo Jen Psaki aliwaambia wanahabari kuwa rais huyo alitoa jibu la moja kwa moja kwa swali la moja kwa moja.
Katika miaka ya hivi karibuni, uhusiano kati ya Marekani na Urusi umezidi kudorora na kumekuwa na wito mjini Moscow kwa Urusi kusimamisha uhusiano wa kidiplomasia. Hata hivyo siku ya Alhamisi Putin alisema kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Marekani katika masuala yalio na faida kwa Urusi.
Matamshi ya Biden yamechochea mzozo mkubwa wa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili huku Urusi ikimuagiza balozi wake nchini Marekani Anatoly Antonov kurejea nchini humo kwa mashauriano muhimu katika hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa katika historia ya sasa ya kidiplomasia. Ubalozi huo umeonya kuwa Marekani imesukuma ukingoni uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.