1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yataka kuhusika katika mchakato wa amani rasi ya Korea

Daniel Gakuba
10 Oktoba 2018

Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema nchi hiyo imekubaliana na China na Korea Kaskazini juu ya kuwepo mazungumzo ya pande tano yatakayohusisha pia Marekani na Korea Kusini katika kumaliza mvutano katika rasi ya Korea.

Russland Moskau Außenministerium
Picha: picture-alliance/dpa/V. Melnikov

Kauli ya hiyo ya Urusi kuhusu amani katika rasi ya Korea imetolewa baada ya mkutano wa manaibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, China na Korea Kaskazini, ambao ulifanyika jana Jumanne mjini Moscow. Tangazo la wizara ya mambo ya nje ya Urusi limesema mkutano huo uliunga mkono mazungumzo ya kuondoa mivutano katika eneo hilo, na kurejesha mahusiano katika hali ya kawaida.

Katika juhudi hizo hizo za kuboresha mahusiano, Korea Kusini imesema inafikiria kuiondolea Korea Kaskazini vikwazo ilivyoiwekea, ili kuupa msukumo mchakato wa kidiplomasia katika kuondoa kitisho cha silaha za nyuklia kwenye rasi ya Korea.

Azma hiyo ya Korea Kusini iliwekwa wazi na waziri wake wa mambo ya nje Kang Kyung-wha, wakati wa ukaguzi wa wabunge kwenye wizara yake. Kang alisema vikwazo wanavyotafakari kuindolea Korea Kaskazini ni vile vilivyowekwa mwaka 2010 kufuatia shambulizi dhidi ya meli ya jeshi la Korea Kusini, ambalo liliuwa wanamaji 45.

Tangu kuingia madarakani kwa serikali ya kiliberali nchini Korea Kusini, mahusiano na Korea Kaskazini yamekuwa yakiboreka.Picha: picture-alliance/dpa/AP/South Korea Unification Ministry

Kufuatia shambulizi hilo la Korea Kaskazini, Korea Kusini ilisitisha biashara zote kwenye mpaka baina ya mataifa hayo pacha, isipokuwa tu viwanda vinavyomilikiwa kwa pamoja katika eneo la Kaesong, ambalo pia lilifungwa baada ya Korea Kaskazini kufanya jaribio la silaha za nyuklia Februari mwaka 2016.

Hatua za Mei 24

Vikwazo vya mwaka 2010 vilivyofahamika pia kama 'Hatua za Mei 24', vilizizuia meli za Korea Kaskazini kutumia njia ya bahari iliyo katika himaya ya Korea Kusini.

Kuondolewa kwa vikwazo hivyo vya Korea Kusini havitaipa ahueni kubwa Korea Kaskazini, kwa sababu vikwazo vikali ilivyowekewa na jumuiya ya kimataifa ikiongozwa na Marekani, vitabaki pale pale.

Hata hivyo ni dhahiri kwamba serikali ya kiliberali ya Korea Kusini inajiandaa kuanzisha tena miradi ya pamoja ya kiuchumi na Korea Kaskazini, ikiwa mazungumzo mapana kati ya Washington na Pyongyang kumaliza mzozo wa kinyuklia yataanza kuzaa matunda.

Akizungumza na wabunge, waziri wa mambo ya nje wa Korea Kusini amesema vikwazo vya nchi hiyo vya mwaka 2010 ndivyo kizingiti kikubwa kinachozuia kuanzishwa tena kwa safari za kitalii kuzuru ''milima ya Almasi'' iliyo Kaskazini, ambazo zilisimamishwa mwaka 2008, baada ya mwanamke kutoka Korea Kusini kuuwa huko.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, rtre

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW