Urusi yatambua rasmi uhuru wa majimbo ya Georgia yaliyoasi
26 Agosti 2008Uamuzi wa Rais Medvedev ulitangazwa baada ya kiongozi huyo kukutana na mawaziri waandamizi na wakuu wa kijeshi kuujadili mzozo wa Georgia na hivyo amepuuza mito ya nchi za magharibi ya kutochukua hatua kama hiyo. Medvedev,katika hotuba iliyotangazwa kwenye televisheni ya taifa alisema,uamuzi huo mgumu umepaswa kupitishwa kwa sababu ya mgogoro wa hivi sasa nchini Georgia.Akaeleza kuwa ametia saini amri ya kutambua uhuru wa Ossetia ya Kusini na Abkhazia kwani hiyo ni njia pekee ya kuokoa maisha ya wakazi wa maeneo hayo. Akatoa wito kwa mataifa mengine pia kufuata mfano wa Urusi na kuongezea:
"Uamuzi huo umepitishwa kwa kuzingatia matakwa ya umma wa Ossetia ya Kusini na Abkhazia na kuambatana na Katiba ya Umoja wa Mataifa, Azimio la mwaka 1975 na vile vile hati za sheria za kimataifa. "
Lakini uamuzi huo umekosolewa vikali na serikali mbali mbali huku Rais wa Georgia Mikheil Saakashvilli akisema uamuzi huo wala hauna thamani kwa sheria ya kimataifa.Kwa upande mwingine,Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema,huo ni uamuzi usiokubalika na usioambatana na sheria ya kimataifa.Ufaransa iliyoshika wadhifa wa urais katika Umoja wa Ulaya imeuhimiza umoja huo kulaani hatua iliyochukuliwa na Urusi.
Wakati huo huo,Katibu Mkuu wa NATO,Jemadari Jaap de Hoop Scheffer katika taarifa iliyotolewa amesema,anapinga kabisa uamuzi wa Urusi kutambua majimbo ya Georgia yaliyoasi.Na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Milliband akipinga vikali uamuzi wa Urusi,ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusimama pamoja kupinga uchokozi wa Urusi nchini Georgia.
Sauti zikiendelea kupazwa kupinga uamuzi uliopitishwa na Urusi,Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Franco Frattini amesema,huo ni uamuzi wa upande mmoja na upo nje ya mfumo wa sheria ya kimataifa.Wakati huo huo waziri mwenzake wa Marekani Condoleezza Rice alipozungumza na waandishi wa habari mjini Ramallah kwenye Ukingo wa Magharibi alisema,uamuzi wa Urusi unakwenda kinyume na baadhi ya maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.Amesema,kuambatana na maazimio ya Baraza la Usalama,Abkhazia na Ossetia ya Kusini ni sehemu ya mipaka ya Georgia inayotambuliwa kimataifa na itaendelea kuwa hivyo.
Japan pia imeeleza wasiwasi wake na imesema,ni matumaini yake kuwa Urusi itachukua hatua zinazowajibika kwa utulivu wa eneo hilo. Kwa maoni ya Sweden uamuzi uliopitishwa na Urusi ni kukiuka kwa makusudi sheria ya kimataifa.Lakini katika miji mikuu ya majimbo ya Abkhazia na Ossetia ya Kusini yaliyojitenga na Georgia,risasi zilifyatuliwa hewani kufurahia uamuzi wa Urusi na watu walimiminika mitaani,wengi wakilia machozi ya furaha.