Urusi yatambua rasmi uhuru wa majimbo ya Ukraine
22 Februari 2022Mgogoro wa Ukraine umechukua sura mpya,sura inayozidisha mashaka juu ya kutokea uvamizi wa Urusi. Jana Rais Vldamir Putin alitangaza kutambua uhuru wa majimbo mawili yanayowania kujitenga na Ukraine na kuvitaka vikosi vya Urusi kwenda kwenye maeneo hayo kuwalinda wananchi.
Hii leo Urusi imetangaza kwamba bado inataka kuendelea kukaa kwenye meza ya diplomasia kuhusiana na Ukraine. Ingawa tangazo hili la Urusi linatolewa katika wakati ambapo jana nchi hiyo ilionesha mwelekeo mwingine kabisa.
Jana Rais Putin alitambuwa rasmi uhuru wa majimbo mawili yaliyotangaza kujitenga na Ukraine,Donetsk na Luhansk. Kabla ya rais Putin kutangaza uamuzi huo viongozi wa majimbo hayo mawili walimtaka kiongozi huyo wa Urusi kuwalinda raia wa majimbo hayo kwa kutambua uhuru wa majimbo hayo.
Kama alivyosikika kiongozi wa jimbo lililojitangazia uhuru wake,la Luhansk,Leonid Pasechnik.
''Mpendwa rais Vladmir Vladimirovich,ili kuzuia vifo vya halaiki vya raia wa jamhuri hii,ambao 300,000 ni raia wa Urusi,nakuomba uyatambue mamlaka na uhuru wa jamhuri ya watu wa Luhansk.''
Wito kama huo ukatolewa pia na kiongozi wa jimbo la Donensk Denis Pushilin,wote wakizungumza mbele ya mkutano maalum wa baraza la usalama la Urusi uliofanyika hapo jana Jumatatu.
Ni miito hiyo iliyomfanya rais Putin moja kwa moja kutangaza kile ambacho katika nchi za Magharibi kinatajwa kuwa ndoto ya jinamizi baya kabisa aliyoitimiza kiongozi huyo wa Urusi kwa wananchi wengi wa Ukraine na nchi za Magharibi.
Rais Putin amesema Ukraine sio nchi kamili na kwamba Urusi imelazimika kuingilia kati kuwalinda raia wenye asili ya Urusi wanaoishi ndani ya maeneo ya mashariki mwa Ukraine dhidi ya mauaji ya kimbari.
Lakini nchi za Magharibi na Ukraine yenyewe wanamlaumu rais huyo kwa kutengeneza hoja kuhalalisha hatua anazozichukuwa, ikiwemo namna mwaka 2014 alivyolinyakuwa jimbo la Crimea.
Lakini pamoja na yote hayo hii leo msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi Maria Zakharova ametoa tamko akisema kwamba hata katika nyakati mbaya kabisa wako tayari kushiriki kwenye mchakato wa kidiplomasia na kuongeza kwamba waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Sergei Lavrov bado anamatumaini ya kukutana na waziri mwenzake wa Marekani Antony Blinken siku ya alhamisi.
Kimsingi mawaziri hao walitakiwa kujadili uwezekano wa kufanyika mkutano wa kilele kati ya rais Vladmir Putin na Joe Biden wa Marekani. Hata hivyo haieleweki hivi sasa ikiwa suala la kufanyika mkutano huo bado liko mezani au la baada ya hatua ya rais Putin. Na Marekani pia inaziongoza nchi nyingi za Magharibi katika mchakato wa kuiwekea vikwazo vikali Urusi.
Duru za karibu kabisa na ikulu wa Urusi zinaeleza kwamba wanajeshi wa nchi hiyo tayari wameshaingia katika jimbo linalozozaniwa la DonBass ambako waasi wa eneo hilo wanaoungwa mkono na nchi hiyo ya Urusi- wamekuwa wakipambana na wanajeshi wa Ukraine tangu mwaka 2014.
Ingawa hakuna taarifa rasmi kutoka Urusi ya kuthibitisha uwepo wa wanajeshi wake katika eneo hilo. Waasi wa jimbo hilo wanatuhumu kwamba wanajeshi wa Ukraine wanawashambulia kwa kuwafyetulia makombora.
Hofu imeongezeka ikionesha uwezekano wa kutokea uvamizi wa Urusi tangu nchi hiyo ilipopeleka maelfu ya wanajeshikatika eneo la mpaka wake na Ukraine mwaka jana. Japokuwa siku zote Urusi imekanusha tuhuma hizo ikisema haina mpango wowote wa kuivamia Ukraine.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Josephat Charo