Urusi yatanua uwanja wa ndege nchini Syria
14 Septemba 2015Shirika la haki za binaadamu la Syria lenye makao yake mjini London, Uingereza limesema vikosi vya Urusi vinajenga barabara ndefu itakayoziwezesha ndege kubwa kutua karibu na uwanja wa ndege wa kijeshi wa Hmaymeen, mkoani Latakia. Shirika hilo limeripoti kwamba Warusi wanawazuia Wasyria, wawe ni wanajeshi au raia, kuingia katika eneo kunakojengwa barabara hiyo.
Kundi hilo limesema katika wiki za hivi karibuni ndege za jeshi la Urusi ziliwasili Hmaymeen zikiwa zimebeba vifaa vya kijeshi na mamia ya washauri wa kijeshi na mafundi wa mitambo. Mkurugenzi wa shirika hilo Rami Abdel Rahman ameripoti kwamba Urusi inatanua uwanja wa ndege wa Hamadiyeh katika mkoa wa Tartus, ngome nyingine ya serikali iliyo kusini mwa Latakia.
Uwanja huo kwa sasa unatumiwa na ndege zinazomwagia mimea dawa za kuua wadudu. Urusi ni mshirika mkubwa wa utawala wa Syria mjini Damascus na ina kituo cha jeshi la majini katika mkoa wa Tartus. Haijaufanya siri msaada wake kwa serikali ya Assad, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuipelekea silaha, lakini imekataa madai ya kuimarisha uwepo wake kijeshi nchini Syria.
Kamanda wa jumuiya ya kujihami ya NATO barani Ulaya, Jenerali wa Marekani Philp Breedlove amesema jumuiya hiyo inafuatilia mienendo ya Urusi nchini Syria kwa wasiwasi mkubwa. "Sisi kama nyinyi tunafuatilia suala hili kwa wasiwasi. Bado hatufahamu hasa Urusi inachotaka kukifanya Syria. Tumesikia kuhusu misaada ya kibinaadamu na operesheni dhidi ya ugaidi. Kinachotutia wasiwasi ni operesheni itakayoendelea kuusaidia utawala wa Assad."
Marekani ina wasiwasi
Madai hayo yanakuja wakati maafisa wa Marekani wakielezea wasiwasi kuhusu Urusi kuongeza shughuli zake za kijeshi nchini Syria, huku rais wa Marakani Barack Obama akiionya Urusi dhidi ya kumsaidia rais Assad.
Maafisa wa Marekani wamesema meli mbili za kivita ziliwasili hivi karibuni katika kambi ya Tartus na kwamba ndege kiasi nne zimetua katika uwanja wa ndege wa Latakia kutokea Urusi. Waliripoti pia kuhusu kuwasili kwa wanajeshi wa Urusi na kujengwa kwa nyumba za muda za kutosha kwa ajili ya mamia ya watu katika uwanja huo, pamoja na vifaa vya kuongoza safari za ndege vinavyoweza kusafirishwa kirahisi.
Urusi kuendelea kuisaidia Syria
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema jana kwamba nchi yake itaendelea kuusaidia utawala wa Assad katika kile alichokiita kuwa ni juhudi zake za kupambana na ugaidi. Lavrov aidha alizikosoa nchi za magharibi kuhusu muelekeo wao kuelekea mzozo wa Syria akisema ni ujinga kulizuia jeshi la Syria katika mapambano dhidi ya kundi la dola la kiislamu. Marekani inaongoza kampeni ya mashambulizi ya kutokea angani dhidi ya Dola la Kiislamu, lakini inakataa kulishirikisha jeshi la Syria.
Akizungumza katika mahojiano ya televisheni Lavrov alisema nguvu imara ya kijeshi nchini Syria ni majeshi ya Assad na kuongeza kuwa viongozi wa mataifa ya magharibi wanasema wakiwa peke yao kuwa Dola la Kiislamu ni kitisho kikubwa zaidi kuliko Assad, lakini wanakataa kusema hivyo hadharani wakihofia kufedheheka.
Mwandishi:Josephat Charo/afp/ape
Mhariri:Daniel Gakuba