1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yateka vijiji viwili Ukraine

29 Agosti 2024

Vikosi vya Urusi vimefanikiwa kuviteka vijiji viwili mashariki mwa Ukraine.

Krieg in der Ukraine
Picha: UKRAINIAN ARMED FORCES/via REUTERS

Ikizinukuu duru za wizara ya ulinzi, mashirika ya habari ya Urusi yamesema leo kuwa vijiji hivyo ni vya Stelmakhivka kwenye jimbo la Luhansk, na Mykolaivka kwenye jimbo la Donetsk.

Mapema asubuhi, uongozi wa jeshi la Ukraine ulisema kuwa vikosi vyake vilikuwa vikiyazuia mashambulizi kwenye eneo la Stelmakhivka.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Radoslaw Sikorski amesema Urusi haiko tayari kwa mazungumzo ya amani na Ukraine, kwa sababu inaendelea kuitaka Ukraine iachie sehemu kubwa ya eneo lake.

Akizungumza na shirika la habari la PAP, Sikorski amesema Urusi inataka kuendelea kuitawala Ukraine, na maadam ni hivyo, Ukraine haitokubali.

Alikuwa anajibu tangazo la Rais wa Ukraine Volodymr Zelensky, aliyesema anataka kuwasilisha mpango wa amani kabla ya uchaguzi wa Marekani mwezi Novemba.