1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi yatoa wito kwa UN na ICRC kukataa mwaliko wa Ukraine

16 Septemba 2024

Urusi imetoa wito kwa Umoja wa Mataifa na Shirika la Msalaba Mwekundu kukataa mwaliko wa Ukraine kushiriki katika ukaguzi wa maeneo ya Kursk nchini Urusi, baadhi ambayo yanadhibitwa na vikosi vya Ukraine.

Vikosi vya Ukraine katika mapigano wakati wa operesheni za kijeshi katika eneo la Kursk mnamo Agosti 20, 2024
Vikosi vya Ukraine katika mapigano wakati wa operesheni za kijeshi katika eneo la KurskPicha: 95th Air Assault Brigade/via REUTERS

Msemaji wa Kremlin Dmitri Peskov amesema leo kwamba wanatarajia kuwa kauli kama hizo za uchochezi za Ukraine hazitakubaliwa na wahusika.

Ukraine yaitaka UN na ICRC kuthibitisha hali katika maeneo ya Kursk

Hii leo, Ukraine iliutaka Umoja huo wa Mataifa na Kamati ya Kimataifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu ICRC kuthibitisha hali katika maeneo ya Kursk nchini Urusi yaliotekwa na vikosi vyake.

Soma pia: Urusi yaushambulia mji wa Lviv magharibi mwa Ukraine

Katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii, waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Andriy Sybiga amesema aliiagiza wizara ya mambo ya nje kuualika rasmi Umoja huo wa Mataifa na ICRC kushiriki katika juhudi za kibinadamu katika eneo la Kursk na kuongeza kuwa Ukraine iko tayari kufadhili kazi hiyo na kuthibitisha uzingatiaji wake kwa sheria ya kimataifa ya kibinadamu.

Urusi yaamuru kuhamishwa kwa watu Kursk

Gavana wa eneo la Kursk Alexei Smirnov amesema kuwa mamlaka imeamua kuamuru kuhamishwa kwa lazima kwa wakazi wa maeneo yanayokabiliwa na hatari ya wilaya za Rylsky na Khomutovsky ambazo ziko umbali wa kilomita 15 na mpaka wa Ukraine.

Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Daniel Roland/AFP/Getty Images

Urusi imewashitaki maafisa wawili zaidi wa jeshi kwa kupokea hongo. Haya yamesemwa leo na wachunguzi, hili likiwa ni tukio la hivi karibuni zaidi katika msururu wa kukamatwa kwa watu wanaohusishwa na madai ya ufisadi katika wizara ya ulinzi.

Soma pia:Putin asema uvamizi wa Ukraine Kursk haujawa na athari

Ivan Populovsky, mkuu wa ofisi ya mwakilishi wa jeshi na msaidizi wake, Grigory Zorin, wanadaiwa kupokea zaidi ya $120,000 kutoka kwa kampuni mbili ambazo zilisambaza bidhaa za umeme na nyaya kwa wizara ya ulinzi.

Washtakiwa wakiri makosa

Kamati hiyo ya uchunguzi pia imesema kwa upande wao, wanaume hao walitarajiwa kulegeza ukaguzi wa bidhaa hizo na kuzipendelea kampuni hizo katika maswala mengine wakati wa utekelezaji wa kandarasi za serikali.

Soma pia:Urusi yavishtumu vyombo vya habari vya Marekani

Kamati hiyo imeongeza kuwa wakati wa uchunguzi, washtakiwa hao walikiri kuwa na hatia pamoja na kuhusika kwao katika uhalifu mwingine kama huo.

Waziri wa mambo ya nje wa Korea kaskazini aelekea Urusi

Mbali na hayo, waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini Choe Son Hui, amesafiri kuelekea Urusi kuhudhuria kongamano la nne la wanawake la Ulaya na Asia (Eurasia) pamoja na la wanawake la mataifa yanayoinukia kiuchumi, BRICS huko Saint Petersburg. Haya yamesemwa leo na ubalozi wa Urusi nchini Korea Kaskazini .

Ubalozi huo umesema hotuba na ushiriki wa waziri huyo umepangiwa wakati wa kongamano hilo litakalofanyika kuanzia Septemba 18 hadi 20.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW