1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yatuhumiwa kuiba utafiti wa chanjo ya corona

17 Julai 2020

Serikali za Magharibi zimewatuhumu wadukuzi wanaoaminika kuwa sehemu ya mashirika ya kijasusi ya Urusi kwa kujaribu kuiba habari muhimu za utafiti wa chanjo ya virusi vya corona

Arcturus Therapeutics, RNA medicines company, researches a vaccine for novel coronavirus (COVID-19)
Picha: REUTERS

Serikali za Magharibi zimewatuhumu wadukuzi wanaoaminika kuwa sehemu ya mashirika ya kijasusi ya Urusi kwa kujaribu kuiba habari muhimu za kibinafsi kuhusu utafiti wa chanjo ya virusi vya corona wakati janga hilo likiendelea kuongezeka kote duniani. Hayo ni wakati Brazil ikitangaza kuwa idadi yake iliyothibitishwa ya maambukizi imepindukia milioni mbili. 

Janga la virusi vya corona limeuwa zaidi ya watu 585,000, kuwaambukiza zaidi ya milioni 13.6 na kuuathiri uchumi wa ulimwengu tangu lilipolipuka mwishoni mwa mwaka jana na matumaini ya ulimwengu yamegeukia chanjo inayoweza kuzuia virusi hivyo. Katika ishara nzuri ya karibuni, vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti kuwa majaribio ya chanjo inayofanyiwa utafiti na Chuo Kikuu cha Oxford yameonyesha kuwa imetengeneza kinga ya mwili dhidi ya kirusi hicho.

Lakini saa chache baadae, Kituo cha Kitaifa cha Usalama wa Mitandao kikasema kundi la wadukuzi kwa jina APT29 liliyalenga maabara ya Uingereza yanayofanya utafiti wa chanjo ili kuiba data muhimu za utafiti. Shirika hilo limesema lina uhakika wa zaidi ya asilimia 95 kuwa wadukuzi hao ni sehemu ya mashirika ya kijasusi ya Urusi na yanalenga kukusanya habari kuhusu utafiti wa chanjo ya COVID-19.

Waziri wa afya wa Ujerumani Jens SpahnPicha: Reuters/F. Bensch

Marekani, Uingereza na Canada zimeituhumu Urusi katika taarifa ya pamoja ya usalama, madai ambayo Urusi imeyakanusha kupitia msemaji wa Ikulu Dmitry Peskov.

Mawaziri wa Afya wa Umoja wa Ulaya walifanya kikao jana mjini Berlin na kusema wana furaha kuwa Halmashauri Kuu ya Ulaya itaunga mkono juhudi za watengeneza chanjo ili kutengeneza chanjo salama na inayofanya kazi. Umoja wa Ulaya pia unapanga kutumia karibu euro bilioni 2 katika ununuzi wa mapema wa chanjo zilizo katika majiribio kwa niaba ya mataifa 27 wanachama. Jehns Spahn ni waziri wa afya wa Ujerumani. "Wimbi la pili, ambalo si jambo lisilowezekana, halitawasili ghafla, lakini tutaliona likija, kama tutaendelea kufanya vipimo na kama tutakuwa waangalifu na makini, na nadhani hivyo ndivyo tulivyo katika mataifa yote 27 wanachama"

Hayo yanajiri wakati idadi inayoendelea kuongezeka Brazil na Marekani, nchi mbili zilizoathirika kabisa ulimwenguni, ikidhihirisha haja ya kupatikana chanjo.

Brazil kufikia jana ilitangaza idadi yake ya maambukizi kupindukia milioni mbili wakati Marekani ikiongeza visa 68,000 katika saa 24 zilizopita na kuweka rekodi mpya ya maambukizi kwa siku moja. 

Wakati virusi hivyo vikiyafagia mabara ya Amerika, Shirika la Msalaba Mwekundu limeonya kuwa Kusini mwa Asia imeanza kuwa kitovu kipya cha janga hilo duniani. India itagonga visa milioni moja hivi karibuni, na watu milioni 125 katika jimbo maskini la Bihar, linalopakana na Nepal, walianza jana kutekeleza amri ya kubaki majumbani kwa siku 15.

(afp,ap)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW