1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaushambulia mji wa Kharkiv baada ya ziara ya Baerbock

11 Januari 2023

Vikosi vya Urusi vimeulenga mji wa Kharkiv nchini Ukraine saa chache baada waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock kufanya kwenye mji huo akiambatana na mwenzake wa Ukraine, Dmytro Kuleba.

Ukraine Krieg, Reportage aus Pivnichna Saltivka (Kharkiv)
Picha: Hanna Sokolova/DW

Taarifa kuhusu hujuma hizo za vikosi vya Urusi zimetolewa na gavana wa mkoa wa Kharkiv Oleg Synegubov kupitia mtandao wa Telegram. Alitumia taarifa hiyo kuwarai watu kwenye maeneo ya mji huo kubakia mafichoni akisema "wavamizi wanavurumisha tena mabomu". 

Hata hivyo hapakuwa na taarifa ya vifo wala majeruhi kutokana na mashambulizi hayo. Mji wa Kharkiv umekuwa ukishambuliwa mara kwa mara tangu kuanza kwa vita lakini hivi sasa makabiliano yamehamia upande wa mashariki tangu vikosi vya Ukraine vilipoukomboa mji huo kutoka mikoni mwa Urusi mwishoni mwa mwaka jana.

Katika wiki za karibuni mji wa Kharkiv umekuwa alama ya ushindi wa vikosi vya Ukraine kwenye vita vinavyoendelea nchini humo.

Baerbock autembelea mji wa Kharkiv na kuahidi msaada zaidi kwa Ukraine 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock (kushoto) akiwa na mwenzake wa Ukraine, Dmytro Kuleba mjini Kharkiv.Picha: Xander Heinl/photothek/picture alliance/dpa

Siku ya Jumanne mwanadiplomasia mkuu wa Ujerumani Annalena Baerbock aliutembelea mji huo akiwa pamoja na mwenzake wa Ukraine Dmytro Kuleba.

Alitumia ziara hiyo ya siri kutoa ahadi ya Ujerumani kuipatia Ukraine msaada zaidi ikiwemo silaha na nyongeza ya fedha ili kufanikisha ununuzi wa vifaa muhimu kwa ajili ya vita.

"Mji wa Kharkiv unadhihirisha jinsi ukombozi ulivyo muhimu na jinsi ilivyo muhimu kuendelea kuleta silaha, kwa sababu kwenye mazungumzo yote iwe ni kwenye hospitali ya watoto, au na wanafunzi, au wanajeshi, mtu anasikia na kuhisi makosa ya kivita na uhalifu dhidi ya binadamu uliotendwa na wanajeshi wa Urusi kwenye eneo hili" Baerbock alikaririwa akisema.

Katika ziara hiyo Bibi Baerbock alipeleka msaada wa jenerata na kitita cha fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya mawasiliano kufanikisha upatikanaji wa huduma ya intaneti kwenye mji huo.

Ukraine yairai Ujerumani kufanya uamuzi wa kupeleka vifaru vya kisasa 

Yumkini zawadi hizo hazikumfurahisha sana mwenyeji mwenyeji wake Bw. Kuleba. Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Ukraine alimtanabahisha bibi Baerbock kuwa Ukraine inatarajia zaidi ya majenereta ya kufua umeme.

Mapambano yamechacha kwenye mji wa Bakhmut Picha: CLODAGH KILCOYNE/REUTERS

Nchi hiyo ingependelea Ujerumani ifikie uamuzi wa kutuma vifaru mamboleo vya kijeshi ambavyo serikali mjini Kyiv imeviomba kwa muda mrefu lakini utawala wa kansela Olaf Scholz bado unajikokota kuvipeleka nchini humo.

"Kwa kukosekana uamuzi hivi sasa, kitu pekee kinachoghadhabisha ni kwamba kadri uamuzi unavyokawia, watu wengi zaidi wanapoteza maisha kutokana na upungufu wa vifaru muhimu kwa jeshi letu." alisema Kuleba.

Licha ya fadhaa iliyoelezwa na mwanadiplomasia huyo wa Ukraine, bibi Baerbock ambaye amekuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu kutoka mataifa ya magharibi kulitembelea jimbo la Kharkiv hakusema lolote juu ya iwapo uamuzi wa kuipatia Ukraine vifaru aina ya Leopard utafikiwa hivi karibuni mjini Berlin.

Huko kwenye uwanja wa vita mashariki mwa Ukraine, vikosi vya Urusi vimeendeleza hujuma zake kwa kuushambulia vikali mji wa Bakhmut.

Eneo lingine linaloshuhudia mapambano makali ni kitongoji cha mkoa wa Donetsk kiitwacho Soledar, kinachofahamika kwa uzalishaji mkubwa chumvi. Rais Volodymyr Zelenskyy amesema kwenye maeneo yote hayo karibu kila kitu kimeharibiwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW