Urusi yaushambulia mji wa Kharkiv na kujeruhi watu 21
22 Septemba 2024Urusi imekishambulia kitongoji kimoja cha makazi ya watu katika mji wa Kharkiv nchini Ukraine, na kuwajeruhi watu 21 wakiwemo watoto watatu. Gavana wa mji huo Oleg Synegubov amechapisha taarifa hizo kupitia mtandao wa Telegram akisema watu wanane wamelazwa hospitalini na wawili wako katika hali mbaya.
Urusi imekuwa ikiulenga mara kwa mara mji wa Kharkiv, ambao ni mji wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine ulioko karibu na mpaka wa Urusi mashariki mwa nchi hiyo. Mji huo ulikuwa na wakazi takribani milioni 1.4 kabla ya Moscow kuanzisha vita vyake mnamo Februari mwaka 2022. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema shambulio hilo linadhihirisha, ni kwa nini vikosi vyake vinahitaji kutumia silaha zinazotolewa na washirika wa Magharibi kushambulia zaidi maeneo ya ndani ya Urusi, ombi ambalo hadi sasa limekataliwa.