Urusi yaushambulia mkoa wa Odesa kwa ndege za Drone
19 Aprili 2023Taarifa iliyotolewa na uongozi wa mkoa wa Odesa imesema kuwa ndege hizo ambazo zilikwepa mfumo wa ulinzi wa anga wa Ukraine, zimeharibu "kifaa cha miundombinu ya umma" Jumanne jioni katika mji huo ulioko katika Bahari Nyeusi. Jeshi la anga la Ukraine limedai kuangusha ndege 10 kati ya 12. Kwa upande mwingine, Ujerumani imetangaza kwamba imepeleka mifumo ya ulinzi wa anga chapa Patriot nchini Ukraine ili kuisaidia nchi hiyo kujilinda na mizinga ya makombora ya Urusi. Mifumo hiyo iliorodheshwa jana katika tovuti ya serikali ya Ujerumani.
Soma pia: Ukraine: Urusi yadai kusonga mbele katika mji wa Bakhmut
Hayo yakijiri zoezi la ukaguzi wa meli limeanza tena chini ya makubaliano ya Umoja wa Mataifa ya usafirishaji salama wa nafaka za Ukrainekupitia bandari za Bahari Nyeusi. Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine Oleksandr Kubrakov, ameandika kupitia ukurasa wa Facebook kwamba "ukaguzi wa meli umeanza tena licha ya jaribio la shirikisho la Urusi kutaka kuingilia makubaliano".
Shirika la habari la Urusi RIA, limeripoti kuwa ukaguzi huo ulikuwa tayari umeanza baada ya siku mbili za mazungumzo, likinukuu taarifa ya ofisi ya uratibu ya Umoja wa Mataifa. Kubrakov, yuko nchini Uturuki kujadili juu ya mpango wa usafirishaji nafaka kupitia Bahari Nyeusi ambao ulikubaliwa na Ukraine na Urusi mwaka uliopita kwa ajili ya kupunguza mgogoro wa chakula duniani.
Soma pia: Urusi na Ukraine kurefusha makubaliano ya nafaka
Urusi inadai kwamba ilikubali kurefusha makubaliano hayo hadi Mei 18 huku Ukraine na Umoja wa Mataifa zikisema makubaliano hayo bado yana siku 60 za ziada na zinajaribu kuhakikisha utekelezaji wake unaendelea. Stephane Dujarric ni msemaji wa Umoja wa Mataifa.
"Kuna watu wengi ulimwenguni wanaotegemea chakula na nafaka zinazosafirishwa, wanaotegemea mbolea na hata kama hawategemei haswa nafaka hizo na mbolea, bado wanategemea bei ya chakula na mbolea duniani zisipande", alisema Dujarric.
Na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov ametoa wito kwa nchi zinazojitambua "kuunganisha nguvu" dhidi ya "vitisho" vya nchi za Magharibi wakati mwanadiplomasia huyo akiendelea na ziara yake katika kanda ya Amerika ya Kusini. Akizungumzia vita vya Urusi nchini Ukraine na waziri mwenzake Yvan Gil mjini Caracas, Lavrov amezitaja nchi washirika za Venezuela, Cuba na Nicaragua kama nchi "zilizochagua njia yake zenyewe".
Lavrov ametoa matamshi hayo wakati Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva akilaani ukiukaji wa uadilifu wa eneo la Ukraine na Urusi na kutoa wito kwa mara nyingine wa upatanishi katika kumaliza vita, mpango wa amani ambao uliokosolewa na serikali ya Ukraine.