Urusi yauteka mji muhimu wa mashariki mwa Ukraine
2 Oktoba 2024Kutekwa kwa mji wa uchimbaji madini ya makaa ya mawe wa Vulgedar, karibu kilomita 50 kusini-magharibi mwa jiji la Donetsk, kunazusha maswali kuhusu uimara wa jeshi la Ukraine kwenye uwanja wa vita.
Taarifa iliyotolewa na jeshi la Ukraine inasema kamandi ya jeshi ilitoa amri kwa wanajeshi na zana za kijeshi kuondolewa kwenye eneo hilo. Hata hivyo, jeshi la Ukraine limedai kuwa lilisababisha hasara kubwa kwa vikosi vya Urusi. Lakini mashambulizi hayo yanamaanisha kulikuwa na tishio la kuzingirwa.
Tangu kuanza kwa uvamizi wake nchini Ukraine, Urusi imekuwa ikijaribu kuuteka mji huo wa Vugledar. Kutekwa kwa mji huo wenye wakaazi 14 elfu ni mafanikio makubwa kwa Urusi katika miezi kadhaa ya vita huko mashariki.
Ukraine imesema inachunguza madai ya jeshi la Urusi kuwapiga risasi wafungwa 16 wa vita karibu na mji wa mashariki wa Pokrovosk. Mwendesha Mashataka wa Ukraine, Andriy Kostin amesema kuwa mauaji na mateso ya wafungwa sio ajali bali ni sera ya makusudi ya jeshi na uongozi wa kisiasa wa Urusi.
Urusi yaondoa uwezekano wa mazungumzo ya nyuklia
Kwa upande wake, Gavana wa jimbo la Belgorod nchini Urusi amesema kuwa raia watatu waliuawa leo Jumatano katika shambulio la droni la Ukraine kwenye eneo hilo la mpakani la Urusi.
Kuhusiana tu na vita huko Ukraine, mahakama ya kijeshi mashariki mwa Urusi iliwahukumu vijana 13 kifungo cha hadi miaka 23 jela kwa makosa ya kuhujumu juhudi za vita nchini. Vijana hao walituhumiwa kuharibu miundombinu za reli na za kijeshi magharibi mwa Urusi.
Huku hayo ya kijiri, Urusi imetangaza leo kwamba haitofanya mazungumzo yoyote ya silaha za nyuklia na Mareakani kwa kile inachotaja kuwa ni msimamo wa Marekani katika upanuzi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.
Vikwazo vipya vya EU dhidi ya Urusi
Wakati huo- huo Umoja wa Ulaya umepanga kuiwekea vikwazo vipya Urusi katika kile unachoelezea kuwa ni hujuma za nchi hiyo kwa mataifa ya umoja huo. Mamlaka katika nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya ikiwa ni pamoja na Ujerumani, Poland, Lithuania, Latvia na Estonia zimeripoti kufichua njama au matukio ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya uchomaji moto yaliyopangwa na Moscow katika miezi ya hivi karibuni.
Maafisa wa Ulaya wanasema wanaamini hatua za Urusi zinalenga kwa kiasi fulani kudhoofisha uungwaji mkono kwa Ukraine wakati vita vya Moscow vikiendelea kwa mwaka wa tatu.