Urusi yazidi kubanwa mgogoro wa sumu dhidi ya jasusi
27 Machi 2018Jumuyia ya kujihami NATO imetangaza kuwafukuza wanadiploamsia saba wa Urusi kuhusiana na shambulizi la sumu dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi nchini Uingereza, ikifuata katika nyayo za mataifa kadhaa ya Ulaya na Marekani ambayo serikali zake zimewatimua wanadiplomasia wasiopungua 124 katika muda wa siku mbili, katika hatua iliofanana na zile zilizochukuliwa wakati wa migogoro ya upelelezi ya enzi za vita baridi.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Borris Johnson, amesema haijawahi kutokea kwa mataifa mengi kuja pamoja kuwafukuza wanadiplomasia wa Urusi, akiitaja timuatimua hiyo kuwa pigo litakaloichukuliwa idara ya ujasusi ya Urusi miaka kadhaa kurekekbisha.
Marekani yaongoza njia
"Tumeungwa mkono kwa maelezo yetu ya kilichotokea Salbury bwana spika. Uliona tamko la NATO, uliona taarifa za marafiki wetu katika Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalaama la Umoja wa Mataifa, na balozi wa Urusi katika Umoja wa Ulaya amerejeshwa pia kama unavyojua," alisema Johnson wakati akijibu maswali bungeni Jumanne.
Marekani iliongoza njia katika hatua hizo zilizoratibiwa baada ya Uingereza kutoa wito wa hatua za kimataifa, kwa kuwatimuwa wanadiplomasia 60 wa Urusi katika pigo jipya kwa uhusiano kati ya Marekani na Urusi. Australia, Canada, Ukrain na mataifa 17 wanachama wa Umoja wa Ulaya yalifuata mkondo huo kwa kufukuza idadi ndogo ya wanadiplomasia.
Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema amefuta vibali kwa wafanyakazi saba wa ubalozi wa Urusi kwenye jumuiya hiyo, na kuongeza kwamba atakataa maombi ya vibali kwa wengine watatu. Stoletenberg amesema hili litatuma ujumbe kwa Urusi kwamba kutakuwa na gharama na madhara kwa mwelekeo wa tabia yao isiyokubalika.
'Ni shinikizo la Marekani'
Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imeonya kuwa hatua hizo zisizo za kirafiki hazitapita bila kujibiwa, huku waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Sergei Lavrov akidai kuwa mataifa hayo yameshinikizwa na Marekani.
"Ni vigumu kukwepa hitimisho kwamba tulikuwa sahihi tulivyosisitiza mara kadhaa kwamba kumebakia nchi chache huru katika Ulaya ya sasa. Pili, mwanadiplomasia moja au wawili wanapofukuzwa kutoka nchi hii au ile, huku nchi hizo zikitunong'oneza masikioni kutuomba radhi, tunajua kwa uhakika kwamba haya ni matokeo ya shinikizo na vitisho, ambavyo kwa bahati mbaya ndiyo zana kuu ya utawala mjini Washington kwa sasa."
Ubalozi wa Urusi mjini Washington umewauliza wafuatiliaji wake kwenye mtandao wa twitter, kupigia kura ubalozi mdogo wa Marekani ambao utapaswa kufungwa, ukiorodhesha balozi ndogo zilizoko Vladivostok, St. Petersberg na Yekaterinburg miongoni mwa zinazoweza kupigiwa kura.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe
Mhariri: Mohammed Khelef