1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yazidi kuishambulia Ukraine kwa Makombora ya angani

18 Oktoba 2022

Watu saba wameuwawa na wengine wamejeruhiwa baada ya Urusi kushambulia kwa mara nyengine tena miji kadhaa ya Ukraine, ikiwa ni wiki moja baada ya wimbi la mashambulizi kama hayo yaliyosababisha mauaji pia nchini humo.

Ukraine-Krieg | Drohnenangriffe auf Kiew
Picha: Vladyslav Musiienko/REUTERS

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameyalaani mashambulizi hayo na kuyaita ya kigaidi dhidi ya raia wa taifa lake. Katika mtandao wake wa Telegram, rais Zelensky amesema adui anaweza kuyashambulia miji nchini humo lakini kamwe hatofanikiwa kuwagawa Waukraine.

Drones za kamikaze zaushambulia mji wa Kiev-Ukraine

Moja ya makombora yaliyovurumishwa mjini Kiev hii leo asubuhi yalilenga jengo la makaazi ya watu na kusababisha vifo vya watu wanne akiwemo mama mjamzito. Maafisa nchini humo wamesema watu kadhaa wameokolewa lakini bado kuna wengi wengine wanaoaminika kukwama huko.

soma zaidi: Ukraine yaomba vikwazo zaidi dhidi ya Iran

Kwa upande wake, waziri wa mambo ya ndani wa Ukraine Denys Monastyrskyy amesema Urusi ilirusha ndege 40 zisizo na rubani nchini humo, 5 kati ya hizo zilianguka mjini Kiev. Wizara ya Ulinzi imesema Moscow ililenga mifumo ya nishati na miundombinu katika mashambulizi yake ya angani na majini hii leo Jumanne.

Rais Zelensky aomba mifumo zaidi ya kujilinda na makombora 

Rasi wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Valentyn Ogirenk/REUTERS

Tangu siku ya Jumapili jioni Ukraine imefanikiwa kuzuwiya droni 37 kushambulia nchini humo hii ikiwa ni kwa mujibu wa rais Zelensky aliyeendelea kuitolea mwito Jumuiya ya Magharibi kuipa mifumo zaidi ya kujilinda dhidi ya makombora ya angani.

"Tulifanikiwa kuharibu baadhi ya makombora na ndege zisizokuwa na rubani. Ndani ya masaa 12  kuanzia saa tatu asubuhi siku ya jumapili tulidungua droni 37. Lakini ili kuhakikisha ulinzi wa anga zetu na kupunguza ugaidi unaofanywa na Urusi tunahitaji zaidi mifumo ya kisasa ya kujilinda na makombora," alisema rais Zelensky

Makombora ya Urusi yaua watu 19 Ukraine

Kando na mashambulizi mjini Kiev kumeripotiwa pia mashambulizi mengine ya angani mjini  Sumy, Dnipropetrovsk na Odessa. Mjini Sumi, watu watatu waliuwawa huku wengine tisa wakijeruhiwa.

Urusi yaendelea kushambulia miji ya Ukraine kwa makombora

01:44

This browser does not support the video element.

Huduma za umeme na maji zimekatika katika miji kadhaa iliyoshambuliwa. Kinu kikubwa cha nyuklia cha Zaporizhzhya kinachodhibitiwa na Ukraine pia kwa mara nyengine tena kilikosa umeme ambao ni muhimu katika shughuli zake. 

Azimio la Baraza Kuu la UN kulaani Urusi lapita kwa kura nyingi

Kampuni ya serikali ya Ukraine inayohusika na nishati ya nyuklia, Energo-atom imeishutumu Urusi kuihujumu Ukraine na dunia kwa ujumla kupitia mashambulizi hayo. Kampuni hiyo imetaka hatua za haraka kuchukuliwa ili kuilinda zaidi Ukraine na kinu hicho cha Zaporizhzhya ambacho ni kikubwa zaidi barani Ulaya.

Chanzo: dpa, afp

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW