1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yazidi kukishambulia kiwanda cha chuma cha Azovstal

4 Mei 2022

Majeshi ya Urusi yameanza kukishambulia kiwanda cha chuma cha Azovstal, sehemu ya mwisho walipo wanajeshi wa Ukraine mjini Mariupol, mji ulioshambuliwa kwa mfululizo wa mabomu tangu uvamizi wa Urusi ulioanza Februari 24.

Pro russische Truppen Ukraine Krieg Azovstal
Picha: ALEXANDER ERMOCHENKO/REUTERS

Mashambulizi katika kiwanda hicho yalikuwa ni sehemu ya msururu wa mashambulizi yaliyofanywa Jumanne kote nchini Ukraine ambapo serikali inasema watu 21 wameuwawa katika eneo la Donetsk mashariki mwa nchi hiyo.

Naibu kamanda wa jeshi la Ukraine la Azov Sviatoslav Palamar amesemaUrusi inakishambulia kiwanda cha Azovstal kwa magari ya kivita na vifaru huku Rais Volodymyr Zelenskiy akisema mashambulizi ya sasa ya Urusi yanaonyesha wazi kwamba Urusi haina lengo la kijeshi.

Watu 101 waokolewa kutoka kwenye mahandaki ya enzi za Sovieti

Jeshi la Urusi limethibitisha kwamba majeshi yake kwa ushirikiano na Waukraine wanaoiunga mkono Urusi na wanaotaka kujitenga wanakivamia kiwanda hicho kwa makombora na ndege huku likiyatuhumu majeshi ya Ukraine kwa kutumia muda uliokuwa umewekwa wa kusitisha mapigano kwa kujihami na kuelekea maeneo watakapofanya mashambulizi.

Watu wakitoka kwenye vifusi katika kiwanda cha chuma cha AzovstalPicha: Azov Special Forces Regiment of the Ukrainian National Guard/AP/picture alliance

Umoja wa Mataifa umesema watu 101 wameokolewa kutoka kwenye mahandaki ya enzi za muungano wa Sovieti chini ya kiwanda hicho cha chuma cha Azovstal kama sehemu ya operesheni ya siku tano.

Kulingana na mratibu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine Osnat Lubrani, watu wengine 58 walijiunga na msafara wao kuelekea mji wa Zaporizhzhia kutoka mji wa Mangush nje ya Mariupol. Lubrani ameonya kwamba huenda kukawa na raia wengi zaidi ambao bado wamekwama katika kiwanda hicho huku akidai Umoja wa Mataifa uko tayari kurudi na kuwaokoa.

Haya yanafanyika wakati ambapo Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya imependekeza vikwazo vipya kwa mafuta ya Urusi kutokana na uvamizi huo wa Ukraine. Haya yamethibitishwa na maafisa katika tawi hilo la utendaji la Umoja wa Ulaya.

Vikwazo hivyo vinaziamrisha biashara zilizoko katika nchi za Umoja wa Ulaya kutonunua mafuta ya Urusi lengo kuu likiwa kusitisha kabisa ununuaji wa bidhaa za Urusi. Hivi ndivyo vikwazo vya hivi karibuni kuwekewa Urusi na mwafaka umepatikana baada ya wiki kadhaa za majadiliano ya ndani katika Umoja wa Ulaya ambapo nchi wanachama zilikuwa zinatafakari hasara ya kiuchumi itakayotokana na hatua kama hiyo.

Umoja wa Ulaya wanunua mafuta ya Urusi yenye thamani ya mabilioni

Kituo cha Utafiti wa Nishati na Hewa Safi CREA, kinakadiria kwamba nchi za Umoja wa Ulaya zimenunua mafuta ya Urusi yenye thamani ya yuro bilioni 46 tangu kuanza kwa vita vya Ukraine.

Wakati huo huo, Rais wa Urusi Vladimir Putin akizungumza kwa njia ya simu na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema, nchi yake iko tayari kwa mazungumzo na Ukraine.

Rais wa Urusi Vladimir Putin (kushoto) na Emmanuel Macron wa Ufaransa (kulia)Picha: Irna

Putin vile vile amemwambia Macron kwamba vikwazo vya nchi za Magharibi kwa taifa lake ndivyo vilivyofanya hali ya usalama wa chakula duniani kuwa mbaya zaidi.

Chanzo: AFP/DPA/APE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW