1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yazidi kuushambulia upande wa mashariki kwa Ukraine

13 Agosti 2022

Jeshi la Urusi limeyashambulia maeneo ya makaazi kote nchini Ukraine leo Jumamosi, huku likidai kusonga mbele licha ya vikosi vya Ukraine kujaribu kujibu mapigo.

Russland - Ukraine Konflikt
Picha: Viktor Antonyuk/SNA/IMAGO

Kombora la Urusi limeushambulia mji wa Kramatorsk usiku wa kuamkia Jumamosi na kuwaua watu 3 na kujeruhi wengine 13.

 Hayo ni kulingana na meya wa mji huo. Kramatorsk ni makao makuu ya vikosi vya Ukraine vinavyopambana mashariki mwa nchi hiyo.

Shambulizi hilo la kombora limetokea siku moja tangu kuvurumishwa kwa makombora mengine 11 kwenye mji huo, ambao ni moja ya maeneo mawili ambayo bado yanadhibitiwa na jeshi la Ukraine kwenye mkoa wa Donetsk.

Mkoa huo ulio katika jimbo la mashariki la Donbas umekuwa kitovu cha hujumu za jeshi la Urusi katika wiki za hivi karibuni.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imedai kwamba vikosi vyake vimechukua udhibiti wa kijiji kimoja kiitwacho Pisky, kinachokutikana nje kidogo ya mkoa wa Donetsk, ambao tangu mwaka 2014 wapiganaji wanaotaka kujetenga wamekuwa wakipambana kuukamata.

Ukraine yasema imefanikiwa kuwadhibiti Warusi kusonga mbele 

Picha: Russian Defense Ministry/AP/dpa/picture alliance

Vikosi vya Urusi na wapiganaji waasi wanaotaka kujitenga kwa mkoa huo wamekuwa wakijaribu kuyakamata maeneo zaidi ya kaskazini na magharibi mwa mkoa huo kwa lengo la kutanua eneo la mipaka la mkoa huo ambao waasi wameutangaza kuwa jamhuri mpya.

Hata hivyo vikosi vya Ukraine vimesema vimefanikiwa kudhibiti hujuma hizo hususani kwa kuwazuia wanajeshi wa Urusi na washirika wake kusonga mbele kuelekea miji midogo ya mkoa wa Donetsk ya Avdiivka na Bakhmut.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imedai kwamba mashambulizi karibu na mji wa Kramatorsk, kiasi kilometa 120 kaskazini wa kitovu cha mkoa wa Donetsk, yameharibu mfumo wa kufyetua makombora ulitolewa na Marekani pamoja na shehena ya vilipuzi.

Sehemu ya Luhansk bado inashikiliwa na Ukraine 

Picha: DW

Hata hivyo mamlaka za Ukraine hazijathibitisha hasara yoyote ya kijeshi katika uwanja wa mapambano lakini zimesema mashambulizi ya makombora ya Urusi kwenye mji wa Kramatorsk yameharibu majengo 20 yanayotumiwa kama makaazi.

Madai ya kila upande hayakuweza kuthibitishwa mara moja na duru huru za habari.

Gavana wa mkoa jirani wa Luhansk, ulio sehemu ya mapigano ya kuwania jimbo la mashariki mwa Ukraine la Donbas na ambao vikosi vya Urusi vilichukua udhibiti wake mwezi uliopita, amedai vikosi vya Ukraine bado vinadhibiti sehemu fulani ndogo ya mkoa huo.

Akiandika kupitia ukurasa wa Telegram, Gavana wa Luhansk Serhii Haidai amesema vikosi vya Ukraine vimejificha kwenye kituo cha kusafisha mafuta pembezoni mwa mji mdogo wa Lysychansk.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW