1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi yazidisha mashambulizi Bakhmut

1 Machi 2023

Vikosi vya Urusi vimefanya mashambulizi makali katika mji wa mashariki mwa Ukraine wa Bakhmut, katika juhudi zao za kupata mafanikio kwenye vita hivyo vilivyodumu kwa mwaka mzima.

Russlands Angriff auf Ukraine | Bakhmut
Picha: Marko Djurica/REUTERS

Mjini wa Bakhmut ulikuwa na wakazi wapatao 70,000 kabla ya vita lakini umeharibiwa vibaya wakati wa miezi kadhaa ya mapigano, ukiwa kitovu cha mashambulizi ya Urusi na vikosi vya Ukraine vilivyodhamiria kuulinda.

"Adui anaendelea kusonga kuelekea Bakhmut. Hasiti kuuvurumishia makombora mji wa Bakhmut, jeshi la Ukraine  lilisema katika taarifa yake ya asubuhi ya Jumatano.

Ikiwa Urusiitafanikiwa kuutwaa mji huo mdogo wa madini, itafungua njia ya kukamata vituo vya mwisho vilivyobaki vya mijini katika Mkoa wa viwanda wa Donetsk.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, katika ujumbe wake wa vidio usiku wa manane jana Jumanne, alisema vita vya Bakhmut vilikuwa vigumu sana lakini utetezi wake ulikuwa muhimu.

"Urusi kwa ujumla haijali watu hata kidogo, inawapeleka kwa wingi katika mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya ngome zetu. Mapigano yanazidi tu makali," alisema Zelenskiy.

Soma pia:kraine yasema kuwa vikosi vyake vipo chini ya shinikizo katika eneo la Bakhmut

Mchambuzi wa masuala ya kijeshi wa Ukraine Oleh Zhdanov alisema vikosi vya Urusi vimekabiliana kati ya vijiji viwili kaskazini mwa Bakhmut, Berkhivka na Yahidne, katika jitihada zao za kuuzingira mji huo.

"Mafanikio haya kwenye ubavu wa kaskazini wa Bakhmut yanaleta tishio la wazi kwetu," alisema katika maoni yaliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii.

Ingawa mashambulizi mengi ya Urusi yalijikita Bakhmut na miji na vijiji vingine vya Donetsk, jeshi la Ukraine limesema vikosi vyake vimezuia mashambulizi 85 ya Urusi kwenye sehemu tofauti za mstari wa mbele katika siku iliyopita.

Jeshi hilo pia lilisema katika taarifa yake jana usiku, kwamba ndege zake za kivita zilishambulia maeneo matatu ya wanajehsi wa Urusi. Shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha taarifa hizo za uwanja wa vita.

Shirika la habari la serikali ya Urusi RIA lilitoa kipande cha video ambacho lilisema kinaonyesha ndege za kivita za Urusi aina ya Su-25 zikiunguruma juu ya Bakhmut.

"Tunafuraha kuwa ni zetu," anasema mwanamume katika klipu hiyo aliyetambuliwa kama mpiganaji wa kundi la mamluki la Wagner, akiongeza kuwa ndege hizo ziliwasaidia "kisaikolojia".

Vita vigumu sana

Mjini Washington, afisa mwandamizi wa ulinzi wa Marekani Colin Kahl alikiambia kikao cha bunge kwamba mambo yalikuwa yalikuwa magumu sana kwenye uwanja wa mapigano, na hakukuwa na ishara kwamba Warusi wanaweza kusonga haraka ndani ya Ukraine na kuteka maeneo makubwa wakati wowote mwaka huu au ujao.

Colin Kahl afisa mwandamizi wa ulinzi wa Marekani Picha: DoD/ZUMA Press/picture alliance

Kahl alizungumza wakati wa kikao kilichojikita kwenye usimamizi wa karibu dola bilioni 32 za msaada wa kijeshi ambao utawala wa Rais Joe Biden umetoa kwa Ukraine tangu uvamizi wa Urusi Februari 24 mwaka jana, ikiwa ni pamoja na ndege zisizo na rubani, mifumo ya mizinga ya masafa marefu, na uwezo wa ulinzi wa anga.

Ukraine imetafuta silaha ili kujikinga na mawimbi ya mashambulizi ya makombora ya Urusi na ndege zisizo na rubani ambazo katika kipindi kikali cha msimu wa baridi ziliharibu gridi ya umeme na miundombinu mingine, kuua mamia ya raia na kuwaacha mamilioni bila umeme wala maji.

Kama sehemu ya uchunguzi wa iwapo mashambulizi hayo yalikiuka mikataba ya Geneva kuhusu mzozo wa kijeshi, mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, Karim Khan, alikuwa Ukraine siku ya Jumanne.

"Kwa ujumla tunaona wazi muundo, nadhani, katika suala la idadi, ukubwa na upana wa mashambulizi dhidi ya gridi za umeme za Ukraine na tunahitaji kuangalia ni kwa nini hilo linafanyika; je, ni shabaha halali au la?" Khan aliwaambia waandishi wa habari katika mji wa Vyshhorod kaskazini mwa mji mkuu wa Kyiv.

Soma pia:Kamanda wa vikosi vya ardhini vya Ukraine asema hali ni ngumu sana katika mji wa Bakhmut

Urusi inasema mashambulizi yake ni halali yanayolenga kudhoofisha jeshi la adui lakini Ukraine inayataja kama njia ya kuwatisha wananchi. Zelenskiy, akizungumza baada ya kukutana na Khan, alisema mahakama hiyo ina jukumu la "kihistoria" katika kuleta haki kwa uhalifu uliofanywa katika vita na kuhakikisha usalama wa muda mrefu.

Mawaziri wa mambo ya nje wakutana

Kwingineko mawaziri wa mambo ya nje kutoka kote duniani wanakutana mjini New Delhi leo Jumatano na kesho Alhamisi, katika kivuli cha uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, mzozo unaozidi kati ya Marekani na China.

Mkutano huo utahudhuriwa na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov na mwenzake wa Marekani Antony Blinken huku China ikitarajiwa kumtuma waziri wake wa mambo ya nje Qin Gang.

India haitaki Ukraine itawale mkutano huo, lakini itaongoza ajenda, alisema afisa wa wizara ya mambo ya nje ya India.

NATO yajadili jinsi ya kuipatia Ukraine silaha zaidi

01:30

This browser does not support the video element.

Soma pia:Mawaziri wa mambo ya nje wa G20 wakutana India

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov Jumanne alirudia msimamo wa Moscow kwamba iko tayari kwa mazungumzo ya amani lakini Ukraine na washirika wake wa Magharibi lazima wakubali unyakuzi wa Urusi wa mikoa ya Donetsk, Luhansk, Kherson na Zaporizhzhia baada ya kura za maoni mwezi Septemba mwaka jana ambazo serikali nyingi zilisema ni kinyume cha sheria.

Licha ya vikwazo kadhaa katika uwanja wa vita katika kile Urusi inachokitaja kama "operesheni maalum ya kijeshi" kulinda maslahi yake ya usalama, vikosi vyake bado vinadhibiti takribani humusi moja ya maeneo katika jirani yake Ukraine inayoegemea Ulaya.

Serikali ya Zelenskiyimefutilia mbali mazungumzo na Urusi na kuwataka wanajeshi wake kuondoka kwenye mipaka ya Ukraine mwaka 1991, mwaka ambao Umoja wa Kisovieti ulisambaratika.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW