Kufuatia mashambulizi ya ndege kwa muda wa saa 24 zilizopita hadi mapema leo, maafisa wa Ukraine wamesema watu 21 wameuawa na kituo kimoja cha polisi kimeharibiwa.
Watu 2,000 wameuawa Ukraine tangu uvamizi ulipoanza
Shirika la kitaifa la Ukraine linalotoa huduma za dharura limesema takriban watu 2,000 wameuawa tangu Urusi ilipoivamia Ukraine wiki iliyopita.
Kwenye ukurasa wake wa Facebook, shirika hilo limesema maafisa 10 wa kutoa huduma za dharura ni miongoni mwa waliouawa.
Urusi imesema imechukua udhibiti kamili wa mji wa bandari Kherson ulioko katika bahari nyeusi. Lakini meya wa mji huo amepinga kauli hiyo akisema wangali imara ndani ya Ukraine.
Hata hivyo maafisa wa pande zote, Ukraine na Urusi wamesema wanajeshi wa Urusi wameingia katika mji wa pili wa Ukraine Kharkiv. Jeshi la Ukraine limeeleza kwamba mapigano yamekuwa yakiendelea katika mitaa ya mji huo wa Kharkiv.
Matangazo
Urusi yaongeza mashambulizi katika miji muhimu
Kufuatia mashambulizi, mashirika ya kutoa huduma za dharura yameripoti kwamba watu wanne wameuawa na tisa wamejeruhiwa mjini Kharkiv.
Urusi imeimarisha mashambulizi yake katika miji ya Ukraine ikiwemo magharibi na kusini mwa Kyiv.
Raia wateseka huku vita vya Ukraine vikiendelea
Huku mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine yakiendelea, raia wanahangaika kuikimbia nchi hiyo. Wengine wamejificha katika makazi ya kujizuia dhidi ya mabomu.
Wakazi wa Kyiv wamekuwa wakitumia njia mbali mbali kurudisha nyuma vikosi vya Urusi. Hapa, washiriki wa ulinzi wa raia wanatengeneza n mchanganyiko wa Molotov.
Picha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance
Kusimama imara
Wakaazi wa Kyiv wameunda vitengo vya ulinzi wa raia kulinda jiji lao na familia zao. Hapa mlinzi wa raia mwenye silaha anapiga doria mitaani huko Kyiv baada ya amri ya kutotoka nje.
Picha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance
Kusubiri kwa uoga
Wale ambao hawawezi kukimbia shambulio la Kyiv wanapata makazi popote wanapoweza kupata kimbilio. Wengi huenda kwenye makao ya chini ya ardhi au vituo vya treni ya chini ya ardhi wakati ving'ora vya mashambulizi ya anga vinapolia.
Picha: Kunihiko Miura/AP/picture alliance
Uharibifu
Licha ya uhakikisho wa Urusi kutolenga majengo ya kiraia, roketi na makombora yametua katika maeneo ya makazi kama jengo hili la ghorofa huko Kyiv, ambalo liliharibiwa mnamo Februari 26.
Picha: Efrem Lukatsky/AP/dpa/picture alliance
Hofu
Mwanamke amesimama nje ya nyumba yake iliyoharibiwa vibaya baada ya shambulio la roketi huko Kyiv mnamo Ijumaa, Februari 25. Vikosi vya Urusi vimewalenga raia katika miji kadhaa kote Ukraini tangu Alhamisi.
Picha: Emilio Morenatti/AP Photo/picture alliance
Mfululizo wa mashambulizi
Wakati wa usiku kuanzia Ijumaa hadi Jumamosi asubuhi, mashambulizi ya Urusi dhidi ya Kyiv yaliendelea. Jengo hili la makazi ya juu katika mji mkuu lilipigwa kwa kombora, kulingana na Meya wa Kyiv Vitali Klitschko. Klitschko amewataka wakazi wa jiji kujiepusha na madhara.
Picha: Gleb Garanich/REUTERS
Kutafuta usalama
Watu wanajificha katika majengo ya chini ya ardhi wakati ving'ora vya kuonya ya mashambulizi mapya vinapigwa mjini Kyiv. Urusi ilianzisha mashambulio la kila upande dhidi ya Ukraine mapema Februari 24.
Picha: Emilio Morenatti/AP/picture alliance
Kituo cha treni ya chini ya ardhi kimegeuka kuwa hifadhi dhidi ya mabomu
Wakazi wa Kyiv pia wamekuwa wakienda kwenye vituo vya treni vya chini ya ardhi ili kukaa salama huku mapigano yakiendelea. Jiji hilo lina idadi ya takriban watu milioni 3.
Picha: Zoya Shu/AP/dpa/picture alliance
Kukimbia eneo la vita
Raia waliohamishwa kwa treni kutoka mashariki mwa Ukraine wanawasili Lviv, magharibi mwa nchi hiyo. Nchi jirani za Poland, Hungary, na Romania zinapokea wakimbizi wengi.
Raia wa Ukraine wakiwa wamebeba mali zao kwenye kivuko cha mpaka cha Astely-Beregsurany, wakitorokea Hungary. Foleni ndefu zimeundwa mpakani, kwani watu waliokatata tamaa wanataka kuondoka.
Picha: Janos Kummer/Getty Images
Mwishowe wapo salama
Wakimbizi wawili wa Ukraine wakikumbatiana wanapowasili Hungary baada ya kupita kivuko cha mpaka cha Beregsurany Februari 26. Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban aliapa kutoa msaada wa kibinadamu kwa waliowasili.
Picha: Bernadett Szabo/REUTERS
Watu wa kujitolea watoa msaada
Wafanyakazi wa kujitolea wanatayarisha sandwichi kwa ajili ya wakimbizi wa Ukraine wanaokimbilia Romania kupitia kivuko cha mpaka cha Siret, Ijumaa, Februari 25. Mamlaka ya Romania imejitayarisha kwa ajili ya kufurika kwa raia wa Ukraine.
Picha: Andreea Alexandru/AP/picture alliance
Hatuendi popote
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, anaendelea kutuma ujumbe wa kuwahimiza raia wa Ukraine waendelee kupinga uvamizi na hivyo kuongeza ari ya wapiganaji wa Ukraine wakati wanajeshi wa Urusi wakilikaribia jiji, na milio mikubwa ya milipuko ilisikika mapema Februari 27.
Waangalizi wanaofuatilia yanayojiri kuhusiana na mzozo huo wameelezea hofu ya uwezekano wa mji mkuu Kyiv kuwa katika hatari ya kushambuliwa Zaidi kufuatia vikosi vya Urusi nje ya mji huo.
Hayo yakijiri, Uhispania ndiyo nchi ya hivi karibuni zaidi kutangaza kuipa Ukraine zana za kivita.
Maafa ya vita
Tangu uvamizi huo kuanza, Ukraine imedai kwamba wanajeshi 5,840 wameuawa. Hata hivyo takwimu hiyo haijaweza kuhakikiwa. Urusi kwa upande wake imekiri kukumbwa na maafa ila haijaweka wazi takwimu kamili.
Kulingana na wizara ya Ulinzi ya Urusi, wanajeshi wake waliharibu zana za kivita 1,500 za Ukrain zikiwemo ndege 58, drones 46 na vifaru 472.
Ukraine imekana kupata hasara hiyo kufikia sasa.
Katika shambulizi la jana Jumanne lililofanywa na Urusi dhidi ya mnara wa kituo cha televisheni cha Kyiv, watu watano waliuawa. Hayo yamesemwa na Ukraine.
Hayo yakijiri naibu waziri mkuu wa Ukraine Iryna Vereshchuk ametoa wito kwa kiongozi mkuu wa kanisa katoliki Papa Francis kuzungumza na rais wa Urusi Vladimir Putin ili afungue njia kuwezesha misaada ya kiutu kupitishwa kupelekewa wahanga wa machafuko.
Kulingana na Umoja wa Mataifa takriban watu 836,000 wameyakimbia machafuko hayo kwenda nchi jirani.