1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yazidisha mashambulizi Kiev

15 Machi 2022

Vikosi vya Urusi vimezidisha mashambulizi yake kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kiev, wakati ambapo wapatanishi wanakutana tena katika duru nyingine ya mazungumzo ya kusitisha mapigano. 

Ukraine Kriegszerstörungen in Kiew
Picha: Cover-Images/imago images

Mashambulizi hayo yaliyofanyika mapema Jumanne asubuhi kwenye maeneo ya makaazi ya watu mjini Kiev, yamewaua takribani watu wawili. Jengo la ghorofa 16 katika wilaya ya Sviatoshynsky na jingine lenye ghorofa 10 kwenye eneo la Podilsk yameshambuliwa katika mashambulizi hayo ya anga. Maafisa wa huduma za dharura wamesema kuwa zaidi ya watu 27 wameokolewa katika mashambulizi hayo.

Urusi yaudhibiti mkoa wa Kherson

Huku hayo yakijiri, jeshi la Urusi limesema limechukua udhibiti kamili wa mkoa wa Kherson kusini mwa Ukraine. Eneo hilo lililoko katika Bahari Nyeusi ni makaazi ya watu wapatao milioni moja. Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi, Igor Konashenkov amesema pia majeshi ya Urusi yamedhibiti maeneo mingine.

''Vikosi vya wanajeshi vya shirikisho la Urusi vimechukua udhibiti kamili wa eneo lote la mkoa wa Kherson. Wakati vikosi vyetu vinaendelea na mashambulizi, vimeliteka pia eneo la makaazi la Stepne. Kundi la wanajeshi wa Jamhuri ya watu wa Luhansk linaendesha operesheni katika wilaya za kaskazini mashariki mwa mji wa  Severodonetsk,'' alifafanua Konashenkov.

Msafara wa vifaru vya vikosi vinavyoiunga mkono Urusi katika mzozo wa Ukraine na Urusi kwenye mji wa Volnovakha, DonetskPicha: ALEXANDER ERMOCHENKO/REUTERS

Katika taarifa yake fupi ya kila siku aliyoitoa Jumanne, Konashenkov amesema mali kadhaa za jeshi la Ukraine zimeharibiwa, ikiwemo ndege za kivita, helikopta na makombora 13.

Urusi ilikuwa inataka kuanzisha jamhuri ya watu wa Kherson, kama ambavyo ilifanya katika mikoa ya Donetsk na Luhansk, mashariki mwa Ukraine ambayo ilitambuliwa na Urusi kama mikoa huru hivi karibuni kabla ya vita kuanza.

Mazungumzo kuendelea Jumanne

Wakati huo huo, wapatanishi wa Urusi na Ukraine wanakutana katika duru nyingine ya mazungumzo ya kusitisha mapigano. Mazungumzo hayo yanaendelea Jumanne kwa njia ya video baada ya mazungumzo ya Jumatatu kusitishwa bila ya kuwepo mafanikio.

Ukraine imesema inataka amani, usitishaji wa mapigano mara moja na kuondolewa kwa wanajeshi wa Urusi. Hata hivyo, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema mazungumzo ya jana yalikuwa mazuri.

Mshauri mkuu wa utumishi katika Ikulu ya Ukraine, Oleksiy Arestovich amesema makubaliano ya amani yanaweza kufikiwa ifikapo mwezi Mei. Amesema huenda vita kati ya Urusi na Ukraine vikamalizika ifikapo mwezi Mei au pengine mapema zaidi, kulingana na maendeleo ya sasa.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel (Kushoto), Rais wa Ukraine, Volodymyr Zekensky (Kati) na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen (Kulia)Picha: UKRAINIAN PRESIDENTIAL PRESS SERVICE/AFP

Ama kwa upande mwingine, mawaziri wakuu wa nchi za Poland, Mateusz Morawiecki, Slovenia, Janez Jansa na Jamhuri ya Czech, Petr Fiala wanapanga kwenda Kiev leo kama ujumbe wa Umoja wa Ulaya kukutana na Rais Zelensky. Serikali ya Poland imesema ziara hiyo ya maafisa wa ngazi ya juu imeratibiwa na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen.

Guterres: Mzozo wa Urusi na Ukraine watishia nchi masikini

Aidha, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameonya kuwa vita kati ya Urusi na Ukraine inaziwinda na kuziweka katika hatari nchi masikini duniani ambazo zinakabiliwa na ongezeko la bei za vyakula, mafuta na mbolea.

Guterres amewaambia waandishi habari kwamba Urusi na Ukraine zinawakilisha zaidi ya nusu ya usambazaji wa dunia wa mafuta ya alizeti na karibu asilimia 30 ya ngano ya dunia na kwamba bei za nafaka tayari zimezidi zile zilizokuwepo lilipoanza vuguvugu la harakati za kudai mageuzi katika nchi za Kiarabu na wakati wa mzozo wa chakula mwaka 2007 na 2008.

(DPA, AP, AFP, Reuters)

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW