Urusi yazidisha mashambulizi Ukraine
24 Mei 2026
Maafisa wa Ukraine wanasema mashambulizi hayo yamejiri mapema leo, saa chache baada ya Rais wa Urusi, Vladimir Putin, kuonya kulipiza kisasi kufuatia mashambulizi ya Ukraine katika maeneo yanayodhibitiwa na Urusi mashariki mwa nchi hiyo.
Jeshi la anga la Ukraine linasema mashambulizi hayo yalihusisha zaidi ya droni 600 na makombora 90, huku ulinzi wa anga ukidai kuzuia sehemu kubwa ya makombora hayo. Rais Volodymyr Zelensky amesema Urusi ilitumia pia kombora la kasi kubwa aina ya Oreshnik, ambalo lina uwezo wa kubeba silaha za nyuklia.
Zelensky, amesema baadhi ya makombora yaliharibu nyumba, shule, soko pamoja na miundombinu ya maji mjini Kyiv. Wakazi wengi walilazimika kujificha katika vituo vya chini ya ardhi huku milipuko mikubwa ikisikika katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Mashambulizi hayo yanafuatia shambulio la droni lililofanywa na Ukraine katika mji wa Starobilsk unaodhibitiwa na Urusi, ambapo Moscow imesema watu kumi na wanane waliuawa.