1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi yatumia kura ya turufu kuisaidia Korea Kaskazini

29 Machi 2024

Korea Kusini imelaani hatua ya Urusi kutumia kura yake ya turufu na kuzuia uwezekano wa kurefushwa muda kwa jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaoichunguza Korea Kaskazini.

Rais Vladimir Putin akiwa na Rais Kim Jong Un
Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un (kushoto) akisalimiana na Rais wa Urusi Vladimir Putin Picha: Vladimir Smirnov/AFP

Wataalamu hao hufuatilia vikwazo vya kimataifa vilivyodumu kwa miaka 15 dhidi ya Korea Kaskazini, kutokana na mipango yake ya silaha za nyuklia.

Serikali mjini Seoul imesema inaonyesha wazi kwamba Shirikisho la Urusi, licha ya hadhi yake kama mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limefanya uamuzi usio na uwajibikaji. China imejizuia kupiga kura katika kikao hicho kilichofanyika hapo jana.

Soma pia: Korea Kaskazini ilipeleka makontena 7,000 ya silaha Urusi

Ukraine na Marekani wamelaani pia hatua hiyo ya Urusi ambayo inajiri wiki kadhaa baada ya chombo hicho kusema kinachunguza ripoti zinazodai kuwa  Moscow na PyongYang zimekuwa zikibadilishana silaha. Katika taarifa ya pamoja baada ya mkutano huo, Marekani, Ufaransa, Korea Kusini, Japan na Uingereza zimetaja kusikitishwa na matokeo ya kura hiyo.