Urusi za Ukraine zaendelea kushambuliana vikali
2 Januari 2026
Urusi imedai kuwa jeshi la Ukraine lilishambulia kwa droni mgahawa mmoja katika kijiji cha Khorly huko Kherson na kuwaua raia 27 wakiwemo watoto wawili ambao walikuwa wakisherehekea Mwaka Mpya huko Kherson . Svetlana Petrenko, msemaji wa Kamati ya Urusi inayofuatilia makosa ya jinai amesema uchunguzi kuhusu mashtaka ya kutekeleza kitendo cha kigaidi umeanzishwa.
Madai hayo yamekanushwa vikali na Ukraine iliyosema kuwa mashambulizi yake hulenga maeneo ya kijeshi pekee, kama alivyosisitiza msemaji wa Jeshi Dmytro Lykhovii kuwa vikosi vya Ukraine vinaheshimu kanuni na sheria za kimataifa za kibinadamu kwa kulenga maeneo ya kijeshi, miundombinu ya mafuta na nishati vya Urusi. Lykhovii ameongeza kuwa Urusi imekuwa mara kwa mara ikitumia taarifa za uongo na upotoshaji ili kuvuruga mchakato unaoendelea wa mazungumzo ya amani.
Mchakato wa mazungumzo waendelea
Shutuma hizo za Urusi zinanajiri huku Marekani ikiendeleza harakati za kidiplomasia za kujaribu kuvimaliza vita hivyo vya karibu miaka minne nchini Ukraine. Mapema wiki hii, Moscow ilisema kuwa msimamo wake katika mchakato wa amani utabadilika kutokana na kitendo cha Kyiv kufanya shambulio la droni na kuyalenga makazi ya Rais wa Urusi Vladimir Putin, madai yaliyokanushwa na idara ya ujasusi wa Marekani CIA.
Ukraine kwa upande wake kupitia rais Zelensky imetaja kuwa mazungumzo hayo yanaendelea na kwamba hadi kudikia mwishoni mwa mwaka 2025, mkataba wa amani ulikuwa umefikia asilimia 90 ili ukamilike, japo kuwa bado kuna masuala yeti yanayohitaji kujadiliwa.
Hayo yakiarifiwa, makabiliano yameripotiwa sehemu mbalimbali hususan katika jimbo la Donetsk ambako raia wanaelezea wanavyoishi na matumaini licha ya vita kuendelea. Maksym Lysenko ni mkaazi wa Kramatorsk anaesema kuwa wanaeneza fikra kuwa Donetsk itakuwa huru licha ya ukweli kwamba kila siku, eneo kubwa la mkoa wao linakaliwa.
"Bado tunaamini kwamba katika siku zijazo, maeneo haya yatarejeshwa," alisema mkazi huyo wa Donetsk.
Katika hatua nyingine, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amemteua hivi leo aliyekuwa mkuu wa idara ya ujasusi wa kijeshi Kyrylo Budanov katika wadhifa wa Msimamizi Mkuu wa utawala wa rais, kufuatia hatua ya Andrii Yermak kujiuzulu zaidi ya mwezi mmoja uliopita baada ya kuandamwa vikali na kashfa ya ufisadi katika sekta ya nishati.
Zelensky amesema kwa sasa Ukraine inahitaji kujikita zaidi katika masuala ya usalama, kuviimarisha vikosi vyake vya ulinzi na usalama, na kujizatiti kidiplomasia katika mchakato wa mazungumzo, mambo ambayo yatasimamiwa na Ofisi ya Rais inayoongozwa sasa na Budanov mwenye umri wa miaka 39 na mmoja wa watu mashuhuri na maarufu zaidi huko Ukraine hasa wakati huu wa vita na Urusi baada ya kuionza idara hiyo ya ujasusi wa kijeshi tangu mwaka 2020.
(Vyanzo: Mashirika)