1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Urusi,Ukraine zaendelea kurushiana mkururo wa droni

Angela Mdungu
21 Januari 2025

Ukraine imesema kuwa Urusi imeishambulia kwa droni takriban 131 usiku wa kuamkia Jumanne. Jeshi la ulinzi wa anga nchini humo limeeleza kuwa hata hivyo lilifanikiwa kuyazuia baadhi ya mashambulizi hayo.

	
Moto uliotokana na madharashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine ukizimwa huko Mykolaiv Ukraine
Shughuli ya kuzima moto baada ya Urusi kushambulia moja ya miji ya UkrainePicha: UKRAINIAN EMERGENCY SERVICE/HANDOUT/AFP

Taarifa ya jeshi la anga la Ukraine imesema, jeshi hilo lilifanikiwa kuzidungua droni 72 kati ya 131 zilizorushwa na Urusi. Limeongeza kuwa droni nyingine 59 lilizorushwa na Urusi zilipotea na kushindwa kuyafikia maeneo zilikoelekezwa.

Kulingana na jeshi hilo la anga la Ukraine baadhi ya majengo yaliharibiwa kwa mashambulizi hayo katika mikoa miwili ya Ukraine, lakini hakuna watu waliojeruhiwa.

Ripoti zinasema kuwa sehemu ya droni za Urusi zimeziharibu nyumba saba katika mji wa Kremenchuk. Droni moja iliangukia nyumba na kusababisha moto.

Soma zaidi: Mapambano makali yaendelea kati ya Urusi na Ukraine

Kwa upande wake Urusi imeeleza kwamba, imezidungua ndege 55 zisizo na rubani zilizorushwa na Ukraine usiku wa kuamkia Jumanne. Imesema pia kuwa, mabaki ya droni zilizozuiwa yalisababisha moto kuzuka katika ghala la mafuta kwenye eneo la mpaka.

Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Urusi imebainisha kwamba droni sita za Ukraine zilidunguliwa katika mkoa wa Voronezh. Gavana wa Mkoa huo hata hivyo amethibitisha kuwa hakuna mtu aliyejeruhiwa, na kwamba wahudumu wa idara ya zimamoto walikuwa wakiendelea na juhudi za kuuzima moto uliosababishwa na kuanguka kwa mabaki ya droni zilizozuiwa.

Urusi yashambulia viwanja vya ndege vya kijeshi Ukraine

Urusi pia imedai kwamba ilivishambulia viwanja vya ndege vya kijeshi vya Ukraine. Wizara ya ulinzi ya Urusi, katika mkutano wake kuhusu yaliyojiri katika saa 24 zilizopita imesema kuwa vikosi vyake vimefanikiwa kuyadhibiti maeneo mawili na kuilenga miundombinu ya Ukraine yakiwemo maghala ya silaha na sehemu ya kutengenezea droni.

Jengo lililoathiriwa kwa mashambulizi ya Ukraine katika mkoa wa Kursk, UrusiPicha: REUTERS

Katika hatua nyingine, mamlaka za mji  wa Komarovsky ulio kwenye mkoa wa Orenburg nchini Urusi zimewataka raia wake kujificha katika maeneo maalumu yenye kinga dhidi ya mabomu kutokana na uwezekano wa kutokea kwa shambulio la droni.

Mji huo una kambi maalumu inayohifadhi makombora ya kimkakati, kulingana na gazeti la Kommersant lililoripoti kuhusu taarifa hiyo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW