1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

US kuongeza misaada Ukraine kabla ya Trump kuingia mamlakani

Angela Mdungu
13 Novemba 2024

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken amesema nchi yake itatoa msaada zaidi wa ulinzi kwa Ukraine kabla ya Rais Donald Trump kuingia mamlakani ifikapo Januari 20.

Antony Blinken
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony BlinkenPicha: Brendan Smialowski/REUTERS

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Antony Blinken yuko mjini Brussels ambapo amekutana na na mwenzake wa Ukraine Andrii Sybiha  na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Mark Rutte. Katika mkutano huo Blinken ameihakikishia Jumuiya ya NATO kuwa utawala wa Rais Biden utaimarisha misaada kwa Ukraine katika miezi michache iliyosalia kabla ya Donald Trump kuingia rasmi madarakani.

Blinken amenukuliwa akisema kuwa, " Tunapoendelea kufanya kazi pamoja kuhakikisha Ukraine inapata inachokihitaji ili kujilinda, Marekani inaendelea kuongeza nguvu. Hivi karibuni tumelazimika kutoa tena dola bilioni nane kwa ajili ya msaada wa kiusalama wa Ukraine. Ilikuwa Septemba. Na tumetoa karibu dola nusu bilioni  wiki kadhaa zilizopita na Rais Biden amedhamiria kuhakikisha kuwa kila dola tunayoweza kuipata inafikishwa kati ya sasa na mwezi Januari."

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ukraine amesema usalama wa nchi yake hauwezi kusubiri kwani vita nchini humo vimefikia katika kipindi kigumu.

Urusi yaishambulia Kyiv kwa makombora na droni

Kwingineko, Mkuu wa utawala jeshi nchini Ukraine Serhiy Popko, amesema makombora kadhaa na droni za Urusi yamedunguliwa katika shambulio lililoulenga mji mkuu Kyiv. Shambulio hilo ni la kwanza kwa miezi kadhaa kuchanganya silaha hizo kwa pamoja kwa mujibu wa jeshi la Ukraine.

Moja ya majengo yaliyoharibiwa kwa mashambulizi ya Urusi nchini UkrainePicha: State Emergency Service of Ukraine/REUTERS

Kutokana na mashambulizi hayo mamlaka katika wilaya ya Brovary Magharibi mwa Kyiv zimeeleza kuwa mtu mmoja alipata majeraha madogo baada ya masalia ya roketi kuanguka na jengo moja liliungua moto.

Jeshi la anga la Ukraine limesema makombora mawili aina ya Ch-101 na mawili ya masafa mafupi yaitwayo Iskandery yamezuiwa wakati wa mashambulizi hayo ya Jumatano. Zaidi ya hapo, droni 37 hadi 90 za kivita zilidunguliwa kote nchini humo. Limeongeza kuwa droni mbili zinaaminiwa kuelekea Urusi na Belarus.

Soma zaidi: Marekani yatangaza msaada wa dola milioni 400 kwa Ukraine

Wakati huohuo, Urusi imesema Kyiv ilihusika katika shambulio lililomuuwa afisa wake baada ya bomu kutegwa chini ya gari katika mji wa Savastopol kwenye rasi ya Krimea inayodhibitiwa na Moscow. Kamati ya upelelezi ya Urusi imesema inayachukulia mauaji hayo kuwa ugaidi na kuwa mlipuko huo ulisababisha kuuwawa kwa mwanajeshi ambaye haikumtaja.

Chanzo kimoja cha kiusalama cha Ukraine hata hivyo kimekiri kuwa Ukraine ilihusika katika shambulio la bomu lililomuuwa afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Urusi katika rasi ya Krimea liliyemtaja kwa jina la Valery Trankovsky.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW